HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 23, 2016

Tume ya Mipango yatembelea Kiwanda cha Vinywaji cha Azam

Meneja anayesimamia Ubora wa Bidhaa, Bibi Lilian Mwashigadi (aliyevaa koti jeupe) akiwaonesha maofisa wa ukaguzi wa miradi kutoka Tume ya Mipango hatua za mwisho za uzalishaji wa juisi katika kiwanda cha uzalishaji wa vinywaji kilichopo eneo la Mwandege Mkoani Pwani.

Na Adili Mhina, Pwani

Tume ya Mipango imetembelea kiwanda cha vinywaji cha Azam kilichoko eneo la Mwandege Mkoani Pwani na kuonesha kuridhishwa na shughuli za uzalishaji za kiwanda hicho ikiwa ni moja ya mikakati ya kutekeleza malengo ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17-2020/21) wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.

Timu ya wataalamu wa Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Tume ya Mipango ilifanya mazungumzo na Meneja anayesimamia ubora wa bidhaa kiwandani hapo, Bibi Lilian Mwashigadi na kuelezwa kuwa kiwanda hicho kipo katika hali nzuri na kinaendelea na shughuli za kuzalisha bidhaa zenye ubora unaotakiwa katika kukidhi mahitaji ya soko. 

Bibi Mwashigadi alieleza kuwa kiwanda hicho ambacho kina jumla ya wafanyakazi 800 ambapo kati hao 500 ni ajira za moja kwa moja (direct labor) na 300 ni ajira zisizo za moja kwa moja (indirect labor) kina mikakati ya kuendelea kupanua soko la bidhaa zake kimataifa ambapo kwa sasa kinauza bidhaa katika nchi za Kenya na Rwanda. 

Kuhusu upatikanaji wa matunda ya kutosheleza kiwanda hicho, Meneja huyo alieleza kuwa hakuna changamoto kwani hapa nchini kuna matunda yenye ubora unaokidhi mahitaji ya viwanda na kiwanda chake kinategemea malighafi hiyo kutoka kwa wakulima wadogo wadogo kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Pamoja na hayo, Bibi Mwashigadi aliongeza kuwa kiwanda chake kimeendelea kununua matunda kwa bei nzuri ambayo inaendana na bei ya kawaida ya soko lengo likiwa ni kuhakikisha mkulima anaona faida ya kujishughulisha na kilimo cha matunda. 

Hata hivyo alitoa wito kwa Tume ya Mipango kuangalia namna ya kutengeneza sera itakayosaida kumnufaisha zaidi mkulima mdogo kwani kwa sasa madalali ndio wanaochukua matunda toka kwa wakulima na kupeleka kiwandani na mkulima anaishia kupata faida kidogo huku madalali wakiendelea kunufaika.

No comments:

Post a Comment

Pages