HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 16, 2016

WALIOUZA KIWANJA CHA SHULE WACHUKULIWE HATUA-MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akiwasalimia wananchi wa kijiji cha Londoluo  waliomsimamisha akiwa njiani kutoka Loliondo kwenda Longido  mkoani Arusha.

ARUSHA, TANZANIA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Bw. Rashid Taka na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bw. Raphael Siumbo kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua watendaji wote watakaobainika kuhusika katika uuzwaji wa kiwanja cha shule ya msingi Waso.

Ametoa agizo hilo Desemba 15, 2016) wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kata ya Waso Wilaya ya Ngorongoro akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Arusha.

Waziri Mkuu alisema Serikali haiwezi kuvumilia kuona watendaji wachache wasiokuwa waadilifu  wanamega kiwanja cha shule na kukiuza kwa maslahi yao, hivyo aliwataka viongozi hao kufuatilia na kumpa taarifa ya hatua za kisheria walizochukua kwa wahusika.

“Mkuu wa wilaya na Mkurugenzi hapa kuna malalamiko ya viwanja fuatilieni viwanja hivyo vinavyolalamikiwa na wananchi ni viwanja gani je hiyo ya kwamba mmeuza viwanja vya shule ameuziwa nani,” alisema.

Aidha, Waziri Mkuu amemtaka Bw. Taka ahakikishe Mkuu wa Idara ya Ardhi, Maliasili na Mzingira, Bw. Switbeth Byorushengo anatekeleza majukumu yake ipasavyo. Ametoa agizo hilo baada ya wananchi kudai Ofisa huyo ameshindwa kufanya kazi na kumuomba Waziri Mkuu aondoke naye.

Alisema Bw. Byorushengo anatakiwa kuhakikisha halmashauri hiyo inapima viwanja vya kutosha na kutoa hati kwa wananchi ili waweze kupata maeneo ya kujenga makazi na shughuli zingine za kijamii.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alimuagiza Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Bw. Byorushengo kuhakikisha halmashauri hiyo inaanza ujenzi wa hospitali ya wilaya na ifikapo Aprili, 2017 awe amepewa taarifa za ulipofikia ujenzi huo.

Kwa upande wake Mkurugenzi huyo alisema tayari wapo katika mchakato wa ujenzi wa hospitali ya wilaya ambapo wametenga sh. milioni 800 za kuanzia.

Akizungumzia kuhusu mgogoro wa ardhi kati ya vijiji vya Tarafa ya Loliondo na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Waziri Mkuu alitoa muda wa siku 30 kwa uongozi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Nchini (TANAPA) wawe wamekamilisha uhakiki wa mpaka huo.

Naye Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambaye ni Mbunge wa Ngorongoro Mheshimiwa William Ole Nasha alimuomba Waziri Mkuu kuwasaidia kutatua mgogoro huo wa ardhi kwa kuwa ni wa muda mrefu na unakwamisha shughuli za maendeleo.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Mrisho Gambo alisema Wilaya ya Ngorongoro inachangamoto nyingi ikiwemo ya ardhi na sasa kuna mgogoro kati ya Kampuni ya Thomson Safari na wananchi ambao wanadai kuwa ardhi hiyo ilichukuliwa kinyemela na mwekezaji huyo bila ya wao kushirikishwa.

Alisema baada ya ziara ya Waziri Mkuu kumalizika mkoani hapa atarudi wilayani Ngorongoro kwa ajili ya kutatua kero mbalimbali ikiwemo ya ardhi na matumizi mabaya ya fedha zinazotolewa na wawekezaji ambazo matumizi yake hayajulikani.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, DESEMBA 16, 2016.  

No comments:

Post a Comment

Pages