Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akitoa maelekezo kwa Mkuu wa Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo, Dkt. Mpamila Madale alipofanya ziara ya kushtukiza katika chuo hicho jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika
Utumishi wa Umma Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw.
Ibrahim Mahumi, akitoa ufafanuzi kuhusu taratibu za kiutumishi kwa Mkuu
wa Chuo na baadhi ya watumishi wa Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo
(hawapo pichani) wakati wa ziara ya kikazi chuoni hapo.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt.
Laurean Ndumbaro akifuatilia maelezo ya Mkuu wa Chuo cha Serikali za
Mitaa Hombolo, Dkt. Mpamila Madale alipofanya ziara ya kushtukiza katika
chuo hicho jijini Dodoma.
Katibu Mkuu,
Ofisi ya Rais, Menejimneti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro,
amemwagiza Mkuu wa Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo, Dkt. Mpamila Madale, kuwachukulia
hatua za kinidhamu watumishi waliohusika kumlipa mishahara hewa kwa miezi 11 aliyekuwa
Mhasibu Msaidizi wa Chuo hicho, Bw. Calvin Mushi na kumpa ruhusa ya kuhamia
kituo kingine cha kazi bila idhini ya Katibu Mkuu Utumishi.
Dkt. Ndumbaro
ametoa maagizo hayo leo baada ya kufanya ziara ya kikazi ya kushtukiza katika
chuo hicho kwa lengo la kubaini sababu za kuendelea kumlipa mshahara mtumishi
huyo.
Dkt. Ndumbaro
amewataja watumishi wanaotakiwa kuchukuliwa hatua kuwa ni pamoja na Mkuu wa
Idara ya Utumishi na Utawala wa Chuo hicho na Afisa Utumishi anayeshughulika na
Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara.
Dkt. Ndumbaro
amefafanua kuwa, watumishi hao wamehusika kuiletea hasara serikali kwa kumlipa
mshahara mtumishi asiyestahili Bw. Calvin Mushi ambaye amehamia Bohari Kuu ya
Dawa (MSD) bila idhini ya mwenye mamlaka ambaye ni Katibu Mkuu Utumishi.
Aidha, Dkt.
Ndumbaro amemwagiza Mkuu huyo wa Chuo kumfukuza kazi na kumfungulia mashtaka ya
kinidhamu Bw. Calvin Mushi kwa kupokea mshahara katika vituo viwili vya kazi
yaani Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) huku
akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.
“Kwa kuzingatia
Schedule A, Ndugu Calvin Mushi
asimamishwe kazi na kufunguliwa mashtaka ya kinidhamu na fedha zote alizochukua
zirejeshwe serikalini,” Dkt. Ndumbaro amesisitiza.
Dkt. Ndumbaro
ametoa wito kwa watumishi wote wa umma nchini kufanya kazi kwa kuzingatia
Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya utumishi wa umma ili kuunga mkono
jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano za kuwaondoa watumishi hewa kwa lengo la
kuokoa fedha za serikali ambazo zingetumika katika shughuli mbalimbali za
maendeleo.
Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawa Bora inaendelea kutekeleza maelekezo ya Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhakikisha watumishi wa umma wanaolipwa
mishahara wanakuwa na sifa stahiki kwa mujibu wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo
ya utumishi wa umma iliyopo.
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
OFISI YA RAIS (UTUMISHI)
TAREHE 10 Septemba, 2018
No comments:
Post a Comment