HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 04, 2016

WAZIRI MKUU AKABIDHI PIKIPIKI KWA VIJANA 200 JIJINI ARUSHA

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi kofia gumu  Roman Mollel ikiwa ni ishara ya kumkabidhi pikipiki katika tukio la kukabidhi pikipiki 200  kwa vijana wa bodboda wa Arusha katika uwanja wa Sheikh Amri Abed jijini Arusha , Desemba 4, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema amekabidhi pikipiki 200 zenye thamani ya sh. milioni 400 kwa vijana 200 wa Jiji la Arusha, ili kuweza kuwakwamua kiuchumi
vijana hao ambao walikuwa wakiendesha pikipiki za watu ambazo hazina tija.

Pikipiki hizo zimechangwa na wadau mbalimbali wa maendeleo mkoani Arusha baada ya Mkuu wa Mkoa huo Bw. Mrisho Gambo kubuni mpango huo ambao umewawezesha vijana kupata pikipiki bila riba wala dhamana.

Waziri Mkuu alikabidhi pikipiki hizo jana jioni (Jumamosi, Desemba 3, 2016) mara baada ya kumaliza kuhutubia maelfu ya wananchi waliohudhutia katika mkutano wa hadhara kwenye uwanja cha Sheikh Amri Abeid.

Baada ya kukabidhi pikipiki hizo, Waziri Mkuu aliwataka vijana kuhakikisha wanakuwa waaminifu kwa kufanya kazi kwa bidii ili pikipiki ziweze kuwasaidia kuwainua kipato.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu alisema  mwananchi yeyote hata kama si mtumishi wa umma anawajibu wa kuiheshimu Serikali na kuitumikia.Hivyo aliwataka vijana hao kuwa waadilifu.

“Serikali ya awamu ya tano imeanza kazi na moja kati ya majukumu yetu ni kuboresha nidhamu ndani na nje ya Serikali hivyo ni lazima ipate heshima yake,”.

“Tumeamua kuwatumikia. Tumeamua kuwahudumia watanzania wote bila ya kujali itikadi zao za kisiasa na kidini na Mheshimiwa Rais anataka kuona wananchi wake akifurahia Serikali yao,” alisema.

Kwa upande wake Bw, Gambo alisema pikipiki hizo zilizokabidhiwa kwa vijana hao
zimetolewa sanjari na bima kubwa (Comprehensive Insurance) kwa vijana 200 ambapo
kila Kata ilitoa vijana wanane.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu alisema zaidi ya sh. bilioni 800 zimetengwa kwa
ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Arusha.

Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani Arusha kwa ziara ya kikazi alisema kati ya fedha
hizo sh. bilioni 476 zitatumika katika ujenzi wa miradi wa maji ili kumaliza kero hiyo.

“Mkoa wa Arusha unakabiliwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji safi na
salama, hivyo fedha hizo zinalenga kumaliza tatizo hilo ambalo limechangiwa na
uharibifu wa mazingira,” alisema.

Alisema kiasi kingine cha sh. bilioni 264 kilitolewa ili kuimarisha upatikanaji wa umeme
wa uhakika katika mkoa huo. “Umeme Arusha hautakiwi kukatikakatika huu ni mji wa utalii. Tanesco imarisheni mtandao wa usambazaji,”.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU

JUMAPILI, DESEMBA 4, 2016.

No comments:

Post a Comment

Pages