Balozi Seif Kushoto akisisitiza umuhimu wa wawekezaji wa Mauritius kuitumia fursa ya uwekezaji iliyopo Zanzibar alipokuwa akimueleza Waziri wa Sanaa na Utamaduni wa Nchi hiyo wa kwanza Kulia.
Balozi Seif akimpatia zawadi za Viungo (Spice), Waziri wa Sanaa na Utamaduni wa Mauritius Bwana Santaram Baboo mara baada ya kumaliza mazungumzo yao. Picha na OMPR, Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesisitiza haja kwa Taasisi na Makampuni ya Uwekezaji ya Visiwa vya Mauritius kuanzisha miradi yao ya Kiuchumi na Biashara Zanzibar ili kuitumia vyema fursa iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika Sekta ya uwekezaji vitega Uchumi.
Aliitaja Sekta ya Utalii Zanzibar kuwa imebarikiwa na mazingira mazuri ya rasilmali mbali mbali zinazotoa nafasi pana kwa Miradi ya Kitalii kama Hoteli pamoja na Usafiri wa Anga kuendelea kuwekezwa.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa msisitizo huo wakati wa mazungumzo yake na Waziri wa Sanaa na Utamaduni wa Mauritius Bwana Santaram Baboo aliyeuongoza Ujumbe wa Viongozi Watano wa Sekta ya Utamaduni kutoka Mauritius uliofika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Alisema Visiwa vya Mauritius vimepiga hatua kubwa kimaendeleo katika Sekta ya Utalii ndani ya kipindi kifupi hatua ambayo Wawekezaji hao hao wanaweza pia kufungua milango ya Uwekezaji hapa Zanzibar katika azma ya kuendeleza ushirikiano wa pande hizo mbili zinazofanana Kiutamaduni.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliueleza Ujumbe huo wa Mauritius kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kuwakaribisha Wawekezaji wa Visiwa hivyo kwa kufunga mikataba ya uanzishwaji wa miradi hiyo wakati wowote kuanzia sasa.
Mapema Waziri wa Sanaa na Utamaduni wa Visiwa vya Mauritius Bwana Santaram Baboo alisema upo uhusiano mkubwa wa Kihistoria unaofanana kati ya Zanzibar na Nchi yake hasa katika masuala ya Utamaduni pamoja na uhifadhi wa urithi wa Kimataifa.
Bwana Baboo alisema Zanzibar kama ilivyo Mauritius kwa uzuri wake wa maumbile katika rasilmali za Baharini inaweza kutumiwa na Wasanii mbali mbali wa Kimataifa kurikodi Vipindi tofauti vinavyoweza Kuelimisha, kufurahisha lakini pia Kuitangaza Zanzibar Kiutalii Ulimwenguni.
Waziri huyo wa Sanaa na Utamaduni wa Mauritius alisema mpango huo pia unaweza kuinyanyua Zanzibar Kiuchumi kama ilivyofanikiwa Nchi yake ambayo kwa sasa imekuwa ikipokea watalii Milioni 1.6 kwa mwaka wakati Visiwa vyenyewe vina Idadi ya wakaazi Milioni 1.3.
Bwana Santaram Baboo alielezea kufurahishwa kwake na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo Zanzibar kiasi kwamba mbali ya kurejea kwao kushawishi Makampuni na Taasisi za Uwekezaji za Nchi hiyo lakini pia na yeye binafsi ameshawishika kutaka kuwekeza katika miradi ya Hoteli.
Waziri wa Sanaa na Utamaduni wa Visiwa vya Mauritius Bwana Santaram Baboo na Ujumbe wake umekuja Tanzania na Zanzibar kwa ziara maalum ya kuangalia maeneo ya uwekezaji ambayo Nchi hiyo inaweza kuyatumia katika kuanzisha miradi ya Kiuchumi itakayoendeleza uhusiano kati ya pande hizo mbili.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
5/12/2016.
No comments:
Post a Comment