HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 27, 2017

Muhimbili Yatoa Msaada wa Vitanda kwa Hospitali ya Wilaya ya Kibiti

 Mhandisi Ngereza akizungumza na waandishi wa habari leo baada ya kukabidhiwa vitanda hivyo na uongozi wa hospitali hiyo. (Picha na John Stephen).
Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga, Mtawa katika hospitali hiyo akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukabidhi msaada huo kwa Halmashauri ya Kibiti.
Baadhi ya wafanyakazi wa Halmashauri hiyo wakipakia vitanda hivyo kwenye gari.
 Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Agenes Mtawa akimkabidhi vitanda Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri ya Kibiti, Ayub Ngereza kutokana na hospitali ya halmashauri hiyo kuwa na upungufu wa vitanda vinavyotumiwa na kinamama wakati wa kujifungua.  Mhandisi Ngereza amepokea msaada wa vitanda hivyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Wilaya ya Kibiti.

Na Joh Stephen

Katika kuendelea kuboresha mazingira ya utoaji huduma ya afya ya uzazi kwa kina mama, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) leo imetoa msaada wa vitanda viwili vya kujifungulia  kwa Hospitali ya Wilaya ya Kibiti mkoani  Pwani.

Akikabidhi vitanda hivyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili , Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga Agnes Mtawa amesema  lengo ni kuboresha huduma za afya na kumuwezesha mama kujifungua katika mazingira salama.

"Wenzetu wanahuitaji mkubwa wa vitanda vya kujifungulia hivyo tumeona tuwasaidie, natoa wito kwa Watanzania watambue kwamba hospitali hizi ni za kwetu na zinawahudumia Watanzania hivyo wale wenye nafasi ya kusaidia ni vema wakafanya hivyo ili kuendelea kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto" amesema Sister Mtawa.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo wa Huduma za Uuguzi na Ukunga tatizo la ukosefu wa vitanda husababisha Mkunga kupata shida wakati mama anapojifungua.

Naye  Mhandisi Ujenzi wa Halmashauri ya Kibiti,  Ayub Ngereza akipokea msaada huo kwa niaba ya Mkurugenzi wa wilaya ya Kibiti, ameushukuru uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa msaada huo kwani utasaidia kuboresha huduma za afya.

Hivi karibuni  Hospitali ya Taifa Muhimbili  ilikabidhi msaada wa vitanda vitano vya kujifungulia  kwa  Hospitali ya  wilaya ya Mafya ambapo  kwa mujibu wa Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo  Abdalah Bhai walihitaji vitanda vitano ambao ulikidhi  mahitaji.

No comments:

Post a Comment

Pages