Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizindua rasmi Jengo la Jumuiya ya Kidini ya Al – Madrasatul Khalid Bin Walyd liliopo Jango’mbe Mjini Magharibi. Picha na – OPMR – ZNZ
Balozi Seif akizindua Mitaala Mipya ya masomo ya Jumuiya ya Al – Madrasatul Khalid Bin Walyd hapo Mtaa wa Jang’ombe Mshelishelini.
Balozi Seif akimkabidhi Katiba ya Jumuiya ya Al – Madrasatul Khalid Bin Walyd Ustaadhi Mohamed Juma mara baada ya kuizindua rasmi kuhu akishuhudiwa pia nyuma yake na Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Hassan Othman Ngwali.
ZANZIBAR
Alisema licha ya juhudi kubwa zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali Kuu kujaribu kudhibiti hali hii lakini vitendo vya udhalilishaji wa watoto wadogo wa kike na kiume bado vimepamba moto katika maeneo mbali mbali nchini.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa wito huo katika hafla maalum ya uzinduzi wa Jengo pamoja na Katiba na Mitaala Mipya ya masomo ya Jumuiya ya Al-Madrasatul Khalid Bin Walyd iliyopo Mtaa wa Jang’ombe Mshelishelini Mjini Zanzibar.
Alisema ni jambo la kusikitisha kuona kwamba vitendo vya udhalilishwaji wa kijinsia dhidi ya watoto wadogo vinavyofanywa pia na baadhi ya Walimu wa Madrasa mitaani ni tabia mbaya isiyostahiki tena kufumbiwa macho.
Balozi Seif alieleza kwamba wazo la kuanzishwa kwa Jumuiya na Mitaala Mipya ya masomo ya Ali- Madrasatul Khalid Bin Walid kwa kiasi kikubwa litaweza kusaidia kuimarisha mafunzo ya Dini pamoja na kujenga Umoja utakaopelekea kupunguza kasi ya vitendo vilivyo nje ya maadili.
Alisema kuanzishwa kwa Jumuiya hiyo ni Ukombozi mkubwa kwa Wananchi na Waislamu wote Nchini kutokana na malengo iliyojipangia ikiwemo kusaidia matibabu ya Wazee, malezi ya Watoto Yatima , huduma za maji safi, usafi wa mazingira sambamba na kutoa msaada katika kipindi cha majanga.
Balozi Seif aliwanasihi wanajumuiya hao kutokubali kutumiwa na wanasiasa na kusahau malengo waliyojipangia ya kidini pamoja na maendeleo ya Vijana wao kwani siasa ni sumu kali yenye uwezo wa kuwavurugia malengo yao.
Alisema uzoefu unaonyesha wazi kwamba mambo mengi yanayofanywa na kutekelezwa na Jumuiya na Taasisi za Kiislamu hukosa utaratibu maalum na matokeo yake huzaa migogoro na mifarakano ya mara kwa mara.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea faraja yake kutokana na Jumuiya hiyo iliyosajiliwa Rasmi Serikalini ikiwa na Katiba pamoja na Mitaala ya kufundishia.
Alisema mfumo huo mzuri ulioanzishwa na Jumuiya ya Al – Madrasatul Khalid Bin Walyd unafaa udumishwe ili Jumuiya hiyo iwe chuo cha kufundishia Jumuiya nyengine hapa Nchini.
Akisoma Risala Katibu wa Jumuiya ya Al – Madrasatul Khalid Bin Walyd Sheikh Mohamed Hamduni alisema wanafunzi na Wazee wa Mtaa wa Jang’ombe Mshelishelini wamefikia hatua ya kuanzisha Jumuiya hiyo ili kuendesha mafunzo ya Dini katika misingi ya sheria na Taratibu zilizowekwa na Taifa.
Sheikh Hamduni alisema upo uhaba wa vyombo vya Dini vinavyohusika na jukumu la Umma katika kusimamia wanafunzi waliomaliza mafunzo yao ya Dini hali ambayo baadhi yao huonekana kutumbukia katika matendo maovu.
Alisema Jumuiya ya Al –Madrasatul Khalid Bin Walyd itakuwa chachu ya kuleta mabadiliko ya roho na imani za Waumini wa Dini ya Kiislamu katika muelekeo wake wa kujaribu kutoa mafunzo kwa ajili ya kuisaidia Jamii kuelekea kwenye maadili mema ya Kiislamu.
Akigusia Jengo la Jumuiya hiyoililonunuliwa kwa nguvu za Wanajumuiya wenyewe pamoja na waumini wakereketwa Katibu wa Jumuiya hiyo alisema lengo Kuu ni kulibadilisha kuwa la Ghorofa hapo baadae ili litoe nafasi pana zaidi kwa wanafunzi watakaokuwa wakipata Taalum.
Aliwaomba Waumini wote popote pale walipo nchini na nje ya Nchi kuunga mkono wazo la Jumuiya hiyo katika kuongeza nguvu za uwezeshaji itakayosaidia lengo la ujenzi huo wa Ghorofa kufanikiwa.
Akimkaribisha Mgeni Rasmi katika Hafla hiyo Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Hassan Othman Ngwali aliupongeza Uongozi na wanajumuiya hiyo ya Al –madrasatul Khalid Bin Walyd kwa kazi kubwa iliyojipangia ya kutoa elimu ya dini itakayofungamana na mafunzo ya maadili mema kwa kizazi cha sasa.
Sheikh Ngwali alisema ongezeko la uanzishwaji wa Jumuiya za Kidini Nchini katika kutoa taaluma ndio njia pekee itakayosaidia malezi bora yatayochangia kupungua kwa maovu katika Jamii.
Alifahamisha kwamba kasi ya maovu inayoonekana kushamiri miongoni mwa Jamii inatokana na vijana wengi kukosa taaluma ya maadili vyuoni na hata maskulini na kupelekea kutumbukia katika matendo maovu yakiwemo yale ya matumizi mabaya ya Dawa za kulevya.
Jumuiya ya Al – Madrasatul Khalid Bin Walyd ya Mshelishelini Jang’ombe imeanzishwa mwaka 2016 baada ya kuwa darasa la kawaida ikiwa na malengo ya kuhifadhisha Quran, kuendeleza Elimu ya Dini na Dunia kulingana na mazingira ya mila za nchi.
Malengo hayo yatakwenda sambamba na Jumuiya hiyo kutoa Matibabu kwa Wazee wagonjwa, malezi ya Watoto Yatima, kutoa huduma za maji safi na salama bure, kufanya usafi wa mazingira, kutoa misaada katika kipindi cha majanga tofauti yanayotokea hapa Nchini.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
17/2/2017.
No comments:
Post a Comment