Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya
MOI Profesa Bakari Lembariti leo amezindua vikao vya Baraza la Tatu la
Wafanyakazi wa MOI katika ukumbi wa IDDI NYUNDO katika halmashauri ya Temeke jijini
Dar es Salaam. Vikao vimehudhuriwa na
zaidi ya wajumbe 50 kutoka katika kila idara, vitengo na chama cha wafanyakazi
wa MOI (TUGHE) na wajumbe wa TUGHE mkoa.
Akizindua Baraza hilo Profesa Lembariti
alisema anampongeza Mh Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe
Magufuli. Alisema " Kwa
niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini MOI Mh Zakia Meghji natumia Fursa hii kumshukuru
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa uongozi
wake uliotukuka na jitihada zake za kuboresha huduma za afya hapa nchini, sote
ni mashahidi".
Aidha, Profesa Lembariti aliwakumbusha
wafanyakazi wa MOI kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia maadili ya utumishi wa
Umma ili kujenga imani kwa watanzania walio wengi ambao wanaitegemea MOI kama
Taasisi pekee inayotoa Tiba ya kiwango cha juu cha rufaa kwenye Tiba ya Mifupa,
upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu.
Pia Profesa Lembariti alisema ni vyema
wajumbe wa Baraza la MOI wakatumia vikao vya Baraza kujadili changamoto
mbalimbali zinazoikabili Taasisi ya MOI na kutafuta muarobaini ili Taasisi ya MOI iendelee kutoa huduma bora
Kwa upande mwingine Profesa Lembariti aliwakabidhi zawadi wafanyakazi
Bora wa MOI kwa mwaka 2015/2016 ambapo Bwana Robert Sere aliibuka kidedea na
kuwa mfanyakazi Bora wa MOI na kujipatia cheti na fedha taslimu kiasi cha Tshs
Milioni 4, nafasi ya pili ikishikwa na Bwana Lucas Machage akijipatia cheti na
kiasi cha Tshs Milioni 2 na nafasi ya tatu ikishikwa na Bi Betty Shila ambaye
alijipatia cheti na kiasi cha Tshs
Milioni 1.5
Kwa upande wake ,akiwasilisha ripoti ya
utendaji wa Taasisi ya Kaimu Mkurugenzi wa MOI Dkt Othman Kiloloma alisema
kutokana na ongezeko kubwa la ajali ambazo zimepelekea ongezeko kubwa la
wagonjwa MOI, Taasisi ya MOI iko kwenye mpango mkakati kabambe wa kushirikiana
na baadhi ya hospitali za rufaa za pembezoni kwa kuwapeleka wataalamu kutoa
huduma katika hospitali hizo na kupunguza kama si kuondoa kabisa wimbi la
wagonjwa wanaopokelewa MOI
Dkt Kiloloma alisema kwamba Taasisi ya
MOI imeendelea kuwa Kitovu cha Weledi katika matibabu ya Mifupa ,Ajali ,Ubongo
na Mishipa ya Fahamu katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na kati ambapo mwaka
2015 MOI ilitoa utafiti bora wa mfupa mrefu wa paja duniani ,ambapo utafiti
uliwasilishwa katika Taasisi ya kimataifa ya upasuaji wa mifupa duniani ya Marekani (AOTA)
Vilevile, Dkt Kiloloma aliwaomba wajumbe
wa Baraza la MOI kutoa michango yenye tija ili kupata matibabu ya changamoto
mbalimbali zinazoikabili Taasisi ili Taasisi iendelee kutoa huduma bora kwa
watanzania
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MOI Prof Bakari Lembariti akihutubia wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa MOI wakati wa Uzinduzi wa Kikao cha Tatu cha Baraza Hilo.
Kaimu Mkurugenzi wa MOI Dkt Othman Kiloloma akiwasilisha ripoti ya Utendaji ya Mwaka 2015/2016.
Makamu mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi MOI Prof Bakari Lembariti akimkabidhi cheti Mfanyakazi bora wa MOI kwa Mwaka 2015/2016 bwana Robert Sere.
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa MOI wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni rasmi Prof Bakari Lembariti.
No comments:
Post a Comment