Wachezaji wa Cameroon na viongozi wa timu hiyo, wakishangilia ubingwa wa AFCON 2017.
LIBREVILLE, GABON
SIMBA Wasioshindika Camaeroon, usiku wa kuamkia leo wametawazwa mabingwa wapya wa michuano ya Mataifa Afrika (AFCON 2017), baada ya kuwachapa Misri ‘The Pharaohs’ katika fainali kali kwenye dimba la Stade de l'Amitie, jijini hapa.
Fainali hiyo ya 31, ilionekana kuwaendea vizuri Misri, ambayo ilitangulia kupata bao kunako dakika ya 22, likifungwa na kiungo anayechezea Arsenal ya England, Mohamed Elneny na kudumu hadi filimbi ya mapumziko ya mwamuzi Janny Sikazwe wa Zambia.
Cameroon ilitandaza soka safi na kumiliki mpira kwa asilimia 67 kwa 33 hadi mapumziko, lakini hilo halikutosha kuwaaminisha wafuatiliaji wa fainali hiyo kama wangeibuka mabingwa, kwani walipoteza nafasi nyingi na kuzua hofu ya kufungwa.
Kipindi cha pili Cameroon iliendelea kutawala mchezo na kujipatia mabao mawili, yakifungwa na Nicolas Nkoulou na Vincent Aboubakar, wachezaji walioanzia katika benchi la nyota wa akiba la Cameroon.
Nkoulou aliyeingia dakika ya 32 kuchukua nafasi ya Adolphe Teikeu aliyepata maumivu ya misuli, alifunga bao la kusawazisha dakika ya 59, akimalizia kimiani kazi nzuri ya Benjamin Moukandjo, na kumtungua kipa Essam el Hadary.
Vincent Aboubakar anayekipiga klabu ya Besiktas ya Uturuki, alipigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la Misri katika dakika ya 88, baada ya kufunga bao akiwa katikati ya mabeki watatu Ahmed Hegazy, Gabr na Ahmed Elmohamady.
Kwa ushindi huo, Cameroon sio tu imelipa kisasi cha kipigo cha fainali kama hiyo mwaka 2008, bali pia wamejikatia tiketi ya kucheza Michuano ya Kombe la Mabara la Fifa, ambalo litafanyika Russia kuanzia Juni 17 hadi Julai 2.
Katika michuano hiyo, Cameroon inayonolewa na Mbelgiji Hugo Broos, imepangwa Kundi B, ikiwa na nchi za Australia, Chile na Ujerumani, huku Kundi A likiwa na mataifa ya Russia, Ureno, New Zealand na Mexico.
Nyota wa kimataifa wa Cameroon, Christian Bassogog alitangazwa Mchezaji Bora wa Mashindano, huku Junior Kabananga wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), akiibuka Mfungaji Bora, akifunga mabao matatu.
Furaha ya ubingwa wa AFCON 2017, wachezaji wa Cameroon wakishangilia
Kiungo wa kimataifa wa Misri, anayechezea Arsenal ya England, Mohamed Elnenny, akishangilia bao lake la uongozi aliloifungia Misri dhidi ya Cameroon.
Wachezaji, viongozi na maofisa wa benchi la ufundi la Cameroon, wakishangilia ubingwa wa AFCON 2017
Mlinda mlango wa Misri, Essam El Hadary kulia, akiwa haamini macho yake baada ya Cameroon kusawazisha bao hilo kupitia Nikolas Nkoulou. Wanaoshangilia ni nyota wa Cameroon.
No comments:
Post a Comment