Jonas Kamaleki na Lilian Lundo- MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametutunuku Kamisheni kwa Makamanda 166 kwa cheo cha Luteni usu leo Ikulu, Jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Jeshi Monduli, Meja Jenerali, Paul Peter Masao, amesema mafunzo hayo ambayo yalianza Februari 15, 2016 yamejumuisha watanzania 200 na wengine 20 kutoka nchi rafiki za Burundi, Kenya, Rwanda na Uganda.
Kati ya wanafunzi hao waliofanikiwa kufuzu mafunzo hayo ni 166 ambapo wanaume ni 143 na wanawake ni 23, wakiwemo makamanda 15 kutoka nchi rafiki, alisema Meja Jenerali Masao.
Aidha wawili kati yao waliteuliwa kuchukua mafunzo hayo nchini Burundi ambapo 59 waliachishwa mafunzo kutokana na sababu mbali mbali.
Kabla ya kutunuku kamisheni Mhe. Rais Magufuli alitoa tuzo kwa maafisa watano waliofanya vizuri zaidi katika mafunzo ambao ni Said Daudi ambaye aliongoza katika mafunzo, wengine ni Shahari Majid, Hassan Mbaga, Lucas Mwitamaksau na Mariam Kayanda ambaye alifanya vizuri zaidi kwa upande wa wanawake.
Hafla hiyo ilipambwa na vikundi mbali mbali vya burudani toka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) vikiwemo vya ngoma na bendi ya Mwenge Jazi.
Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi kilianza mwaka 1969 hapa jijini Dar es Salaam, kikifahamika kama Chuo cha Maafisa wanafunzi Kurasini na baadaye kuhamishiwa Monduli Septemba, 1976. Tangu chuo hiki kimehamishiwa Monduli hii ni mara ya pili kwa Mhe. Rais Magufuli kutunuku Kamisheni Ikulu, Dar es Salaam badala ya Monduli.
Kabla ya kuanzishwa kwa chuo hiki maafisa wanafunzi walichukulia mafunzo yao katika nchi rafiki ikiwemo Cuba, Canada, China na Misri.
No comments:
Post a Comment