HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 02, 2017

YOUNG AFRICANS YAAGIZWA KUMLIPA KOCHA BRANDTS

Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA), limeitaka Klabu ya Young Africans ya Dar es Salaam kulipa mara moja deni la aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Ernst Wilhelmus Johannes Brandts - Raia wa Uholanzi waliyevunja naye mkataba miaka miwili iliyopita.

Klabu ya Young Africans imetakiwa kulipa dola 11,000 za Marekani kama ambavyo iliamriwa Juni 30, 2015 na Kamati ya Hadhi ya Wachezaji ya FIFA.

Kwa kuchelewa kulipa fedha hizo tangu Juni, 2015 Klabu ya Young Africans imeamliwa pia ilipe fidia ya asilimia tano ya deni halisi.

Young Africans wametakiwa kulipa fedha hizo na kutuma nakala ya malipo hayo, kabla ya shauri hilo halijapelekwa Kamati ya Nidhamu.

Kutolipa deni hilo kwa wakati, imetafsiriwa kwamba Klabu ya Young Africans imevunja Kanuni ya 64 inayozungumzia Nidhamu katika FIFA yaani FDC (FIFA Disciplinary Committee).

Klabu (Young Africans) inakabiliwa adhabu za kupigwa faini zaidi ya awali, kukatwa pointi katika Ligi Kuu ya Vodacom inayoendelea kwa sasa au kushushwa daraja.

Kamati hiyo ya Nidhamu inatarajiwa kukutana wakati wowote wiki ijayo na suala la Nidhamu ya Young Africans litakuwa ajenda ili kama Young Africans hawakulipa, watachukua hatua kama adhabu zinavyojieleza hapo juu

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeagizwa haraka kufuatilia suala la deni hilo katika Klabu ya Young Africans na kurudisha majibu FIFA. TFF kupitia Katibu Mkuu, imeagizwa kupeleka barua ya FIFA katika Makao makuu ya Klabu hiyo, yaliyoko kwenye makutano ya mitaa ya Jangwani na Twiga, Dar es Salaam.

TFF tumeliweka wazi suala hilo kama ‘Tahadhari kabla ya hatari’, kwani tungeweza kufanya mawasiliano kati ya shirikisho (TFF) na klabu (Young Africans) kwa siri tu, lakini ikitokea huko mbele klabu inakutana na adhabu mojawapo, lawama hushuka TFF kwa madai kwamba tumekalia taarifa muhimu ya kuchukuliwa hatua haraka.

Tunaagiza uongozi wa Young Africans, kulifanyia kazi jambo hilo mara moja kwa utekelezaji.

MECHI ZA WIKIENDI HII LIGI KUU YA VODACOM TANZANIA BARA

Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea leo Februari 2, mwaka huu ambako Mwadui itaialika Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mwadui, Shinyanga.

Mchezo huo pekee Na. 201 utaanza saa 10,00 jioni na Ijumaa Januari 3, Young Africans ya Dar es Salaam, itaikaribisha Stand United ya Shinyanga kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Jumamosi Februari 4, mwaka huu kutakuwa na mechi mbili.

Mechi za Jumamosi  zinatarajiwa kuwa ni kati ya Mbeya City na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya wakati Majimaji itakuwa mwenyeji wa Simba katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Majimaji mjini Songea.

Jumapili kutakuwa na mchezo kati ya Azam FC na Ndanda FC kwenye Uwanja wa Chamazi ulioko Mbande – mchezo unaotarajiwa kuanza saa 1.00 usiku.

Jumatatu kutakuwa na mchezo mmoja tu ambako Toto Africans ya Mwanza itaikaribisha Ruvu Shooting ya Pwani kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Wikiendi ya Februari 10, 11 na 12 hakutakuwa na mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom badala yake wawakilishi wa Tanzania katika mchuano ya kimataifa Young Africans (Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika - CL) na Azam (Kombe la Shirikisho - CC) watakuwa na mechi na mechi za kimataifa.

No comments:

Post a Comment

Pages