HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 03, 2017

HATIMAYE MBUNGE LEMA APATA DHAMANA

NA GRACE MACHA, ARUSHA

MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema, (CHADEMA), ameachiwa kwa dhamana na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha akiwa amesota mahabusu kwa zaidi ya miezi minne ambapo ameahidi kutoa waraka maalum  kwa Rais, John Magufuli.

Aidha, wananchi waliokuwa mahakamani hapo jana walimpokea mbunge huyo kifalme mara baada ya kuachiwa kwa dhamana kwa kumtandikia nguo kwenye njia aliyotumia kutoka kwenye ofisi za msajili wa mahakama hiyo mpaka eneo ilipo bendera ya Taifa alilotumia kuongea na wananchi.

Lema akiongea kwa kujiamini na wananchi hao akiwa ameambata na mke wake, Neema Lema, Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Dkt Vicent Mashinji alisema kuwa ameanda waraka kwa ajili ya Rais, Magufuli, juu ya mateso ya watu wanayoyapa wakiwa gerezani ambao anatazamia kuutoa hivi karibuni.

"Namshukuru Mungu kwani Jamhuri ilinikusudia mabaya lakin Mungu alinikusudia mema, namshukuru sana mke wangu, (Neema Lema), naishukuru sana familia yangu, mawakili wangu viongozi wangu wa chama ambao niko nao hapa leo, nikisema nianze kuongea sitaweza nina waraka nimeuandaa kwa ajili ya mheshimiwa Rais, na nitautoa hivi karibuni kwa siku ambayo nitawatangazia.

"Nimeona mateso mengi ya watu na nafasi hii haiyoshi kwa  sababu mara ya mwisho mtoto wangu aliniuliza baba nifanye kosa gani ili nije nilale na wewe magereza naomba nikamuone kwanza yeye na naomba nikamshukuru Mungu," alisema Lema.

UAMUZI 

Akitoa uamuzi wa kumwachia Lema kwa dhamana  Jaji wa mahakama hiyo, Salma Maghimbi, alisema kuwa baada ya kupitia hoja za mawakili wa pande zote mbili aliowataka wajibu swali la iwapo mahakama ya hakimu kazi Arusha ilikuwa sahihi kisheria kuwaruhusu upande wa jamhuri kusimama kutoa notisi ya dhamana wakati ambapo ilikuwa hajamaliza kutoa uamuzi kwa kuweka masharti ya dhamana.

Alisema kuwa amebaini kuwa mahakama hiyo ya chini  iliruhusu kuingiliwa mamlaka yake kwani ilipaswa kusoma uamuzi wake mpaka uishe pamoja na kuweka masharti ya dhamana ndipo iwape nafasi upande wa jamhuri kuwasilisha notisi yao.

Jaji Maghimbi aliifuta notisi hiyo ya kukata rufaa aliyosema haikuwa sahihi kisheria pamoja na kuitupia mbali rufaa ya jamhuri ambayo ilipangwa  kusikilizwa jana kwani  haiwezi kubaki mahakamani ikiwa haina notisi ya kukata rufaa.

Kwenye rufaa hiyo mawakili wa Jamhuri walikuwa  wakipinga Lema kupewa haki ya dhamana kwa kile alichodai kuwa usalama wake utakuwa hatarini hoja waliyoiwasilisha wakiambatanisha na kiapo cha Mkuu wa upelelezi wa Mkoa, (RCO).


Jaji alisema kuwa kutokana  na kuwa Lema amekaa muda mrefu aliamua  kutumia mamlaka ya mahakama hiyo kisheria ya kuzisimamia mahakama za chini kwa kuamua kuweka masharti ya dhamana ya kumtaka ya kumtaka Lema ajidhamini mwenyewe pamoja na wadhamini wengine wawili watakaosaini hati ya sh milioni moja kila mmoja.


MBOWE

Mwenyekiti wa TaifaChadema, Mbowe alikemea matukio ya jeshi la polisi kuzuia wananchi wasiingie mahakamani huku wakiwapiga na kuwaumiza wananchi waliokuwa wakipita barabara hiuo ya mahakama ambapo wengine waliwapeleka kituo cha polisi.

Alisema kuwa ataenda kulizungumzia suala hilo bungeni kwani haoni sababu ya polisi kuigeuza mahakama kama kituo cha polisi kwa kuzui watu kuingia kwenye chombo hicho cha kutoa haki.

"Ninamkaribisha Lema kwenye majukumu yake ya kibunge ndani ya jimbo lake, ndani ya bunge na ndani ya chama kama Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama, Leo Kamati Kuu ya chama imemaliza vikao vyake ilivyokuwa inavifanya jijini Arusha.

"Hakutakuwa na tukio lolote la kisiasa siku ya leo, natumis nafasi hii kulaani sana jeshi la polisi kwa sababu wamewapiga sana vijana wa Chadema nje. Wamewapiga vijana wanaopita njia wamewaonea sana wamewapeleka watu rumande wamewaumiza watu bila sababu za msingi.

"Huyu ni mbunge wa watu ni lazima watu wampokee, sasa polisi wanapotumia nguvunna mamlaka yao kuumiza raia ni jambo ambalo halikubaliki kwa hiyo mimi nitamtafuta RPC na RCO wa mkoa wa Arusha kuwaambia wajibu wao ni kulinda usalama wa raia na mali zao na si kuwaonea raia," alisisitiza Mbowe.


KIBATALA ALIA TENA

Wakili  wa Lema, Kibatala alionekana akilia huku akiongea kwa shida mara baada ya Jaji kutangaza kumuachia kwa dhamana mteja wake ambapo na yeye aliondoa mahakamani hapo rufaa yao namba 126/2016 ambayo waliifungua mahakamani hapo wakidai mahakama ya hakimu mkazi ilishindwa kutumia vema mamlaka yake kwa kushindwa kumalizia uamuzi wake na kuuruhusu upande wa Jamhuri kuwasilissha kusudio uamuzi wa mahakama ya hakimu mkazi mteja wao kuendelea kushikiliwa wakati

Akiongea nje ya mahakama alisema kuwa anashukuru wameweza kupata haki waliyoipigania kwa muda mrefu mahakamani na wameweza kutimiza ombi la mteja wao aliyewataka wapigane kuhakikisha kumbukumbu hiyo inaondolewa mahakamani ili isije kutumika kuwaumiza wananchi wengine.

Alisema kuwa kwa sasa wamejipanga kuendelea kumpigania mteja wao kwenye mashauti mengine manne ya jinai yanayo mkabili kwenye mahakama ya hakimu mkazi.

MKE WA LEMA ASHINDWA KUONGEA 

Mke wa mbunge wa Lema, Neema , muda wote mahakamani hapo alionekana akilia hukunakikumbatiana na watu mbalimbali ambapo alisema hayuko tayari kuingea chochote.

BABA YAKE LEMA

Baba yake Lema, Jonathan Lema aliwataka wananchi wasikate tamaa huku akdai kuwanaliamini iko siku mwanaye ataachiwa huru kwani makosa yaliyokuwa yakimkabili yana dhamana.
Kutoka kushoto ni Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ambaye pia Mjumbe wa kamati Kuu ya Chadema, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na katibu Mkuu wa Chadema, Vicent Mashinji wakiwa Mahakamani. (Picha zote na Grace Macha).
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, akiwa na mke wake, Neema, baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kumpatia dhamana. (Picha na Grace Macha).
Mbunge wa arusha Mjini Godbless Lema akizungumza na Waandishi wa Habari.
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, (Chadema), akisindikizwa na askari magereza kwenda kwenye ofisi ya msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kukamilisha taratibu za dhamana. 
Mbunge Lema akitoka Mahakamani.
Mbunge Lema akilakiwa na familia yake alipowasili nyumbani kwake.
Ilikuwa ni furaha tupu.
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), akiwa amemkumbatia mtoto wake baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kumpatia dhamana jana. 

Viongozi Wakuu wa Chadema wakiwa na mbunge Lema (wa nne kushoto), nyumbani kwake baada ya kuapata dhamana. (Picha na Grace Macha).
Baadhi ya viongozi wa Chadema wakiwa na mbunge Lema (wa nne kushoto), nyumbani kwake baada ya kuapata dhamana. 
Viongozi Wakuu wa Chadema wakiwa Mahakamani jana. 
Viongozi wa Chadema.
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika akiwa Mahakamani.
 Viongozi wa Chadema wakiwa Mahakamani wakati wa kusikiliza Rufaa ya mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.

No comments:

Post a Comment

Pages