HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 27, 2017

POLISI WAWILI WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA SHTAKA LA KUIBA MAFUTA YA NDEGE

Na Mwandishi Wetu

WATU wanne wakiwemo Askari Polisi wawili, wamepandishwa kizimbani kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakituhumiwa kuiba mafuta ya ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).

Askari hao ni F.8419 CPL, Bahati Msilimini (33) na F.9901 PC Benaus (34).Wengine ni Mlinzi wa Kampuni ya Moko, Iddy Nyangas (42) pamoja na fundi ndege, Ramadhan Mwishehe (52).

Kwa pamoja watuhumiwa hao walisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa na wakili wa serikali mwandamizi, Nassoro Katuga akishirikiana na Leornad Chalo, ambapo walidai wanakabiliwa na kosa moja. 

Wakili Katuga alieleza kuwa kwa pamoja washtakiwa wanakabiliwa na kosa la kula njama, ambapo inadaiwa walilitenda Machi 1, mwaka huu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Inadaiwa kuwa kwa pamoja na makusudi walikula njama ya kutenda kosa la uhujumu. Katika shtaka jingine, inadaiwa kuwa wanakabiliwa na kosa la uhujumu uchumi ambalo walilitenda kati ya Machi 1 na 17, mwaka huu.

Inadaiwa kwa pamoja wakiwa na nia ovu ya kuihujumu serikali ya Tanzania, waliiba mafuta lita 280.6 ya ndege za Shirika la (ATCL), huku wakijua itasababisha usumbu katika shirika hilo kutoa huduma kwa wananchi.

Baada ya kusomewa maelezo hayo, Hakimu Nongwa aliwataka washtakiwa hao kutojibu chochote kutokana na kosa la uhujumu uchumi linalowakabili.

Wakili wa utetezi, Martin Ruhembiza aliiomba mahakama hiyo kuwapa masharti ya dhamana washtakiwa kwa sababu yanadhaminika na hayajafika kiwango cha Sh.milioni 10, pia Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hajawasilisha hati ya pingamizi ya dhamana.

Alidai kuwa mahakama hiyo ina mamlaka chini ya kifungu cha 39 (4) (a) cha sheria ya uhujumu uchumi ambapo kinaipa uwezo mahakama kutoa dhamana kwa kesi ya uhujumu uchumi isiyozidi Sh.milioni 10.

Hata hivyo, wakili Katuga alieleza kuwa suala la dhamana halihusiani na uwepo wa hati ya DPP, bali inategemeana na kosa linalowakabili washtakiwa ni la aina gani.

Kutokana na mvutano huo, Hakimu Nongwa alitoa uamuzi na kusema kuwa washtakiwa hao watapewa masharti ya dhamana kwa kuwa makosa yanayowakabili yapo chini ya Sh.milioni 10.

Pia muundo wa hati ya mashtaka inairuhusu mahakama hiyo kuwapatia washtakiwa masharti ya dhamana.

Hakimu Nongwa aliwataka washtakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh.milioni moja kwa kila mmoja, pia hawapaswi kutoka nje ya Dar es Salaam na kwenda kwenye maeneo yao ya kazi bila kibali maalum.

Washtakiwa hao walitimiza masharti hao.Kesi imeahirishwa hadi Aprili 17, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

Pages