HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 31, 2017

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI UFAFANUZI JUU YA “UZUSHI” ULIOENEA KWENYE MITANDAO YA KIJAMII KUHUSU KUFUKUZWA NCHINI RAIA WA KENYA, WILAYANI LONGIDO, MKOA WA ARUSHA.

Kumekuwepo taarifa ambazo zimekuwa zikiripotiwa kupitia Vyombo mbalimbali vya Habari pamoja na mitandao ya kijamii kuwa, Serikali ya Tanzania inafanya operesheni maalum inayolenga kuwaondoa Raia wa Kenya wanaoishi nchini bila kuwa na Vibali halali huko Wilayani Longido, Mkoa wa Arusha, huku wakimhusisha Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu katika utekelezaji wa ‘zoezi’ hilo.

Taarifa hizi zimezua tafrani na kutishia hali ya usalama iliyopo katika mpaka wa Tanzania na Kenya, Namanga.Tunapenda kutoa ufafanuzi kuhusu Taarifa hizo zinazoendelea kuenezwa kuwa:-

1.    Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haijafanya operesheni yoyote inayolenga kuwakamata na kuwaondoa nchini raia wa Kenya au Taifa lolote lile wanaoishi katika Wilaya ya Longido Mkoani Arusha kama inavyoenezewa kwenye Vyombo vya Habari na Mitandao mbalimbali ya kijamii.

2.    Shughuli za udhibiti wa raia wa kigeni wanaokiuka Sheria za Uhamiaji nchini hazifanywi kwa kulenga Taifa lolote lile, bali hufanywa kwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi. Wahusika wanaokiuka Sheria, Kanuni na Taratibu za uhamiaji hukamatwa na kuchukuliwa hatua kwa makosa yao binafsi na sio kwa msingi wa utaifa wao.

3.    Kukamatwa kwa raia wa kigeni ambao walibainika kuwa ni raia wa Kenya ni sehemu ya shughuli za kawaida za Idara ya Uhamiaji kama Chombo cha Ulinzi na Usalama katika kuhakikisha kwamba raia wa kigeni wanatambuliwa na kuishi kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi.

4.      Suala la kukamatwa kwa raia hao wa Kenya ambao walibainika kukiuka Sheria ya Uhamiaji nchini halihusiani kwa njia yoyote ile na Serikali ya Tanzania kulenga kuwakamata raia wa nchi yoyote na wala si agizo la Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ilivyoripotiwa, bali ni utaratibu wa kawaida ambao unafanywa na nchi yoyote katika kuhakikisha kwamba ukaazi wa wageni unazingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi husika. Kwa mfano, katika mwezi Februari 2017, Idara ya Uhamiaji imewakamata wageni 396 kutoka mataifa mbalimbali kwa makosa ya kiuhamiaji na kuwachukulia hatua mbalimbali kwa mujibu wa Sheria.

5.      Tanzania na Kenya tunao uhusiano mzuri sana ambao ni wa kihistoria na nchi hii ni mwanachama mwenzetu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa uhusiano huo, wapo watanzania wengi wanaokwenda nchini Kenya kwa sababu mbalimbali kama vile matembezi, biashara, masomo nk. Pia wapo raia wengi wa Kenya wanaoingia na kuishi hapa nchini kwa sababu kama hizo hizo na hatuna tatizo nao, alimradi hawavunji Sheria za nchi yetu.

6.    Mwisho, tunatoa wito kwa Wageni wote wanaoishi hapa nchini kwa shughuli mbalimbali kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za uhamiaji nchini. Wapo baadhi ya wageni wanaoingia nchini kihalali, lakini wanaendelea kuishi nchini hata baada ya muda waliopewa kuishi nchini kumalizika. Aidha, wapo baadhi ya wageni wengine wanaoingia nchini kinyume cha sheria na kuendelea kuishi nchini kinyume cha Sheria. Wale wanaobainika kukiuka Sheria, Kanuni na taratibu za uhamiaji nchini watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria bila kujali utaifa wao.

7.    Taarifa zinazoenezwa kupitia Vyombo vya Habari na Mitandao ya kijamii kwamba Tanzania inawalenga raia wa Kenya, kuwakamata na kuwaondoa nchini si sahihi na zipuuzwe kwani zinalenga kuchafua na kuzorotesha uhusiano mzuri uliopo baina ya nchi zetu mbili na wananchi wake, pamoja na kudhoofisha shughuli za udhibiti wa wahamiaji haramu nchini.

8.    Tunafahamu kuwa Tanzania haiwezi kuishi kama kisiwa. Hivyo, tutaendeleza na kuimarisha ushirikiano na Mataifa mengine pamoja na kuendelea kuweka mazingira mazuri kwa wageni kuja na kuishi nchini kwa shughuli mbalimbali, zikiwemo biashara, uwekezaji, utalii, matembezi na nyinginezo.   

Imetolewa na;

KITENGO CHA UHUSIANO,
MAKAO MAKUU, IDARA YA UHAMIAJI,
BARABARA YA LOLIONDO, KURASINI,
 S.L.P 512, DAR ES SALAAM.
31 MACHI, 2017.

No comments:

Post a Comment

Pages