RT wajivunia matokeo Nyika Dunia
NA MWANDISHI WETU, ARUSHA
MSAFARA wa Timu ya Taifa ya Mbio za Nyika iliyoshiriki mashindano ya Dunia huko Kampala Uganda, imerejea nchini juzi jioni huku ikijivunia matokeo iliyoyapata licha ya kutopata medali.
Msafara wa timu hiyo uliokuwa chini ya Meneja Metta Petro, uliwasili jijini hapa majira saa 12:00 jioni kwa basi maalumu lililotolewa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), na kupokelewa na baadhi ya wadau wa mchezo wa riadha na waandishi wa habari.
Akizungumza mara baada ya kuwasili, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday, alisema si sahihi kusema Tanzania imetoka kapa katika mashindano hayo, kwani nafasi ya saba katika matokeo ya jumla kati ya nchi 59 zilizoshiriki mashindano hayo si jambo la kubeza.
Gidabuday, alisema vijana walijitahidi kadri ya uwezo katika mbio hizo zilizokuwa na ushindani mkubwa na kwamba timu ya wanawake senior ilikamata nafasi ya sita na kujitwalia dola 4,000 za Marekani, wanaume senior nafasi ya saba, wanaume Junior namba sita, wanawake Junior nafasi ya 15 na Relay nafasi ya nane.
“Kwa matokeo haya si ya kubeza ni ya kujivunia licha ya kutopata medali kwa mchezaji mmoja mmoja…Nafasi ya saba kidunia sio jambo dogo, michezo mingapi inaota kupata nafasi kama hii katika viwango vya kidunia, hivyo tunawapongeza vijana wetu na pia wamepata mambo mengi ya kuwafunza na kuwajenga kimchezo,” alisema Gidabuday.
Kwa upande wake Meneja wa timu, Petro, alisema licha ya changamoto ndogondogo zilizojitokeza ikiwamo kusafiri kwa muda mrefu zaidi ya saa 36, lakini kiujumla kuanzia kambi hadi ushiriki wa timu ulikwenda vema.
Naye alisisitiza kuwa, matokeo waliyoyapata si ya kubeza, kwani vijana walipigana kwa kiwango chao licha ya changamoto za kiushindani walizokutana nazo kutoka kwa nchi nyingine shiriki.
Aliupongeza uongozi wa RT kwa kuhakikisha kuanzia kambi ya vijana ya wiki tatu hadi jushiriki unakwenda vema, pia Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), kwa kufanikisha ushiriki wa timu hiyo.
Kwa upande wake Emmanuel Giniki ambaye katika mbio za Km. 10 senior alionyesha ushindani mkubwa katika mizunguko miwili ya mwanzo, alisema alishindwa kuendeleza ushindani baada kupata maumivu ya mguu baada ya kukanyangwa na kutobolewa na msumari wa kiatu cha kukimbilia cha mmoja wachezaji wenzake.
Wachezaji walioiwakilisha nchi katika mashindano hayo ni Emmanuel Giniki, Bazil John, Gabriel Gerald, Fabiano Joseph (Nahodha), Josephat Joshua, Wilbardo Peter na Silivestre Simon kwa upande wa Senior huku kwa wanawake ni Magdalena Shauri (Nahodha Msaidizi), Angelina Tsere, Failuna Abdi, Sara Ramadhani, Siatha Kalinga na Mayselina Mbua.
Junior wanaume walikuwa ni Francis Damiano, Yohana Sulle, Ramadhani Hamis, Elisha Wema, Anthony Wema na Joshua Elisante huku kwa wanawake ni Asha Samwe, Amina Mgoo, Noela Khaday, Elizabeth Ilanda na Shamima Salum huku Mixed Relay ni Faraja Damas, Marco Sylivestre, Sicilia Ginoka, Jackline Sakilu.
Nashauri Tanapa na wadau wengine wanaohitaji kusaidia timu zetu waanze na maandalizi hususan kambi za uhakika za muda mrefu ili kuwaweka sawa wachezaji, na sio kufika siku ya kukabidhiwa bendera na ndio mnatangaza udhamini na kutoa jezi na vifaa vingine, naamini hii timu ingeandaliwa mapema ingefanya vizuri sana
ReplyDelete