HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 02, 2017

WAZIRI MKUU APOKEA TAARIFA YA LOLIONDO

*Tumedhamiria kumaliza migogoro nchini

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea taarifa ya Kamati Teule ya Kushughulikia Mgogoro wa Loliondo na kuahidi kuifanyia kazi pamoja na mawaziri husika.

Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Machi 2, 2017) katika kikao alichokiitisha ofisini kwake mjini Dodoma ili kupokea taarifa ya Kamati Teule ya Kushughulikia Mgogoro wa Loliondo. Aliiunda Kamati hiyo, Desemba mwaka jana, mara baada ya kumaliza ziara ya kikazi mkoani Arusha.

Kiini cha mgogoro huo ni eneo la pori tengefu la Loliondo ambalo linagombewa na wawekezaji, wakulima, wawindaji kwa sababu ni mapitio ya wanyama, chanzo cha maji, mazalia ya wanyama, malisho ya mifugo na makazi.

Akizungumza na wajumbe wa kamati hiyo, Waziri Mkuu amesema Serikali imedhamiria kumaliza migogoro yote inayowakabili wananchi katika maeneo mbalimbali nchini ukiwemo wa Loliondo uliodumu kwa miaka 25.

Kamati hiyo inayoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Mrisho Gambo ilikuwa na jukumu la kufanya mapitio ya nini kinachosababisha kuwepo kwa migongano katika eneo hilo ili Serikali itoe uamuzi wenye tija.

“Hatuwezi kuwa tunagombana miaka na miaka bila ya kuwa na solution, hilo hatuwezi kuendelea nalo lazima tushirikiane kumaliza migogoro. Nataka nchi nzima iwe na amani na utulivu,“ amesema.

Waziri Mkuu amesema Serikali imedhamiria kumaliza migogoro hiyo ili kutoa fursa kwa wananchi kuendelea kushiriki shughuli nyingine za maendeleo.

“Wananchi ndio tegemeo letu na tunataka kuona wakinufaika na Serikali yao.Na Serikali haiko tayari kuona migogoro hiyo ikiendelea. Natumaini timu hii itatuwezesha kumaliza mgogoro huu,“ amesema.

Pia Waziri Mkuu amewataka wadau wote katika maeneo mbalimbali nchini wahakikishe wanadumisha amani na washirikiane vizuri na Serikali na inapotokea dosari wasiingize ushabiki usiokuwa na tija.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewaagiza Maofisa Mifugo katika halmashauri zote nchini wahakikishe wanashiriki shughuli za wafugaji ili kujua idadi ya mifugo na changamoto zinazowakabili.

Waziri Mkuu amewataka Maofisa mifugo wawasimamie shughuli za wananchi husasan wafugaji kwa kuonyesha mahitaji ya mifugo iliyoko katika maeneo yao na kuyafanyia kazi.
Awali akiwasilisha taarifa hiyo Bw. Gambo alisema mgogoro huo ulioanza mwaka 1992 ulikuzwa na makundi mbalimbali kutokana na manufaa yao binafsi.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
ALHAMISI, MACHI 2, 2017.


No comments:

Post a Comment

Pages