HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 21, 2017

HAJJI MANARA KUWEKWA KITI MOTO NA KAMATI YA MAADILI

Kwa mujibu wa Katiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kila mwanafamilia wa mpira wa miguu Tanzania analazimika kuheshimu na kufuata kanuni za maadili za shirikisho kama zilivyoainishwa kwenye kanuni zake mbali mbali.

Wanafamilia wa mpira wa miguu ni pamoja na wachezaji, makocha, waamuzi, viongozi wa mpira wa ngazi zote na waajiriwa wa taasisi ambazo ni wanachama wa TFF wa ngazi mbalimbali.

Ili kutunza heshima ya mpira wa miguu Tanzania, wanafamilia wa mchezo huo katika kutimiza masharti ya kanuni za maadili za TFF, hawana budi kuheshimu na kufuata taratibu zote hizo ndani na nje ya uwanja.

Taswira njema ya shirikisho inajenga imani ya wadau wakiwamo serikali, mashirika mbalimbali ya umma na binafsi, vyombo vya habari, vyama vya mpira vya kimataifa, NGO’s na watu binafsi kwa taasisi (TFF). Kinyume chake ni kulibomoa shirikisho.

Dhima ya uongozi wa TFF ni pamoja na kulinda na kutunza heshima hii. Hivyo vitendo vyovyote vyenye viashiria vya uvunjaji wa maadili havitavumiliwa, na vikitokea hatua zitachukulia.

Na kwa muktadha huu Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania, limemfungulia mashtaka ya kinidhamu Msemaji wa Simba Bw. Hajji Manara (pichani) kwenye Kamati ya Maadili. Leo hii Aprili 21, 2017 atapewa mashtaka yake na kujulishwa lini na wapi yatasikilizwa.

TFF inaendelea kutoa rai kwa wadau wa mpira kuwa pamoja ni kwamba ni haki yao kushauri, kupendekeza, kukosoa lakini yote haya yafanyike kwa staha ili kutunza heshima ya mpira wetu.



YOUNG AFRICANS, TANZANIA PRISONS KUMALIZIA ROBO FAINALI ASFC

Mchezo wa Robo Fainali ya Nne ya Kombe la Shirikisho la Azam (Azam Sports Federation Cup 2016/2017), kati ya Young Africans na Tanzania Prisons FC utafanyika kesho Aprili 22, 2017 saa 10.00 jioni kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo utatoa mshindi ambaye ataungana na timu nyingine tatu ambazo tayari zimefuzu kwa hatua ya Nusu Fainali. Timu zilizotangulia Nusu Fainali ya ASFC ni za Mbao FC, Simba SC na Azam FC.

Jumapili Aprili 23, mwaka huu kutakuwa na droo ya wazi kwa timu nne zitakazokuwa zimefuzu kwa hatua ya Nusu Fainali ya ASFC, itakayofanyika Kituo cha Televisheni cha Azam ambao ni wadhamini wakuu wa jina la michuano na haki ya kuonesha mubashara michuano hii ambayo inafanyika kwa msimu wa pili mfululizo.

Azam FC ilikata tiketi ya kucheza Nusu Fainali ya ASFC baada ya kuifunga Ndanda FC mabao 3-1, kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam Aprili 5, 2017 ikitanguliwa na Mbao iliyoishinda Kagera Sugar mabao 2-1 katika mchezo ulifanyika Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera Machi 18, 2017 ilihali Machi 19, mwaka huu Simba iliwatoa Madini ya Arusha kwenye mchezo uliofanyika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Nusu Fainali inatarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu, kabla ya fainali ambako Bingwa wa michuano hii ambayo msimu huu ilishirikisha timu 86 ikiwa ni pamoja na za Ligi Kuu ya Vodacom (timu 16); Ligi Daraja la Kwanza (timu 24); Ligi Daraja la Pili (timu 24) na mabingwa wa mikoa timu 22, atazawadiwa Sh. 50 milioni na kupata tiketi ya kuiwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho - CAF.
…………………………………………………………………….………………………

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA

No comments:

Post a Comment

Pages