HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 03, 2017

Msama: Tamasha la Pasaka si biashara

NA MWANDISHI WETU

MWENYEKITI wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Pasaka, Alex Msama amesema kama angekuwa anaandaa matamasha hayo kwa kigezo cha faida  fedha, tamasha hilo leo hii lisingekuwepo.
Msama alisema ukweli ni kwamba, kama malengo ya Tamasha hilo yangekuwa ni kibiashara kwa maana ya kupata faida, tamasha hilo lisingeweza kudumu hata miaka miwili kwa sababu hakuna faida ya moja kwa moja ya kifedha.
Msama alitoa kauli hiyo juzi alipotakiwa kueleza nini hasa manufaa ya tamasha hilo ambalo kwa mwaka huu linafanyika mara ya 17 tangu mwaka 2000 na kusema manufaa yake ya msingi ni kufikisha ujumbe wa Neno la Mungu.
 “Mimi nimekuwa nikitumia fedha kutoka katika vyanzo vyangu vingine kabisa kufanikisha Tamasha la Pasaka kwani kuleta waimbaji wa nje na wale wa hapa nchini, ni gharama kubwa ambayo huwa hairudi hara kidogo,” alisema Msama.
Alisema akiulizwa kama anapata manufaa yoyote kwa kuratibu Tamasha la Pasaka, jibu ni ndio, lakini si manufaa ya kifedha, bali kutimiza kiu yake ya  kuyafanikisha malengo ya msingi ya uanzishwaji wa Tamasha hilo.
Akifafanua zaidi, Msama alisema mbali ya kufikisha ujumbe wa Neno la Mungu kwa watu wengi kupitia tamasha hilo, pia ni kutumia sehemu ya fedha iliyopatikana kufariji makundi maalumu kama yatima, wajane na walemavu.
Alisema manufaa mengine ni tukio hilo kuchangia kukua kwa muziki wa injili, kukuza vioaji vya waimbaji chipukizi kupitia kupata uzoefu iwe kupewa nafasi ya kuimba jukwani ama kwa kujionea waimbaji wa kimataifa wakihudumu.
“Lakini, nikiri Mwenyezi Mungu hajawahi kuniacha bure. Mara nyingi nimekuwa nikiandaa tamasha katika mazingira magumu kifedha, lakini baada ya tukio hili kupita. Mara nyingi Baraka za Mungu zimekuwa zikijitokeza kwangu,” alisema.
Alisema kitendo cha tukio hilo kuwaleta waimbaji wa ndani na nje ya nchi mbele ya maelfu ya wadau wa nyimbo za injili, ni jambo kubwa ambao yeye na Kamati yake wamekuwa wakijivunia bila kujali wameingiza kiasi gani.



  
    


No comments:

Post a Comment

Pages