Na
Bushiri Matenda na Thobias Robert-Maelezo
Chama
cha kutetea Abiria Tanzania (CHAKUA) kimemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kutoa maelekezo rasmi kwa Mamlaka ya
Usimamizi wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini
(SUMATRA) kuharakisha uanzishwaji wa mfumo wa ukataji tiketi kwa njia ya
kielektroniki.
Mwenyekiti
wa CHAKUA Taifa, Hassan Mchajama, ametoa kauli hiyo leo, Jijini Dar es Salaam
wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu hasara inayoipata Serikali kwa
kutotumika kwa tiketi za kielektroniki kwa vyombo vya usafiri.
Mchajama
amesema kuwa chama hicho kimekuwa mstari wa mbele kuelimisha Umma pamoja na
kuzungumza na mamlaka husika juu ya umuhimu wa kuwa na mfumo bora wa utoaji huduma
ikiwemo suala zima la ukataji wa tiketi za mabasi kwa njia ya kielektroniki.
“CHAKUA
tunaamni kuwa suluhisho la kuwaondolea abiria kero na usumbufu wa kuibiwa, kulanguliwa
tiketi, kudhalilishwa na wapiga debe na kuuziwa tiketi feki liko katika kuanza kwa
matumizi ya mfumo wa ukataji tiketi kwa njia ya kielektroniki,” alisisistiza Mchajama.
Kupitia
mfumo wa kielektroniki utawezesha Serikali kukusanya mapato yake kwa uhakika kuliko
ilivyo sasa na kumsaidia mtumiaji wa huduma kununua tiketi popote alipo na
kuepusha adha zinazojitokeza sasa kwa abiria.
Pia
chama hicho kimepongeza juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano katika kuleta
mabadiliko makubwa na yenye tija kwa Taifa ikiwemo kufunguliwa kwa Kituo maalum
cha kuhifadhi kumbukumbu za matumizi ya malipo na utoaji risiti kwa mfumo wa Kielektroniki.
Aidha
Mchajama amesema kuwa, Serikali inapoteza takribani shilingi milioni 300 kila baada
ya miezi mitatu kutokana na kutotumika kwa tiketi za kielektroniki kwa wasafiri
wa mabasi.
Mwenyekiti
huyo alitoa wito kwa wadau wote wanaohusika na usafirishaji wakiwemo SUMATRA, TRA,
Jeshi la Polisi, TABOA kwa pamoja waweze kushirikiana katika kuharakisha mchakato
wa uanzishwaji wa mfumo huo.
Chama
cha CHAKUA kimekuwa kikikutana na wadau mbalimbali wa usafirishaji na kuwaeleza
changamoto zinazowakabili abiria katika sekta ya usafirishaji wa nchi kavu na
majini hapa Nchini, ukiwemo urasimu unaofanyika katika ununuzi wa tiketi ambapo
kwa sasa wanalazimika kununua tiketi moja kwa moja kwa mawakala na wapiga debe,
ambapo wengi wao wamekuwa wakiwatapeli abiria.
Hivyo
basi, kwa kuanzishwa mfumo wa kielektroniki utaondoa adha hiyo kwa abiria na Serikali
kukusanya mapato kwa uhakika na kuiwezesha Serikali kutoa huduma bora kwa jamii
na maendeleo kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment