WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ametoa miezi mitatu kwa wananchi wote waliojenga
ndani ya eneo la mpaka wa Tanzania na Zambia kubomoa nyumba zao .
Pia
ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuanza kuweka alama za X
katika nyumba 252 zilizojengwa ndani ya mpaka huo ili wahusika
wazibomoe.
Agizo hilo amelitoa leo jioni (Ijumaa,
Julai 21, 2017) alipotembelea eneo la ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha
Forodha (OSBP) katika mpaka wa Tanzania na Zambia, ambacho kinajengwa na
Serikali ya Tanzania na kitagharimu sh. bilioni 12.
“Kuna
watu wamejenga ndani ya mpaka wa Tanzania na Zambia na kuendesha
biashara zao jambo ambalo ni kinyume cha sheria na linazikosesha
Serikali mapato.”
Kufuatia
hatua hiyo Waziri Mkuu ametoa muda wa miezi mitatu kwa watu wote
waliojenga kuanzia umbali wa mita 50 kutoka Tanzania na mita 50 kutoka
Zambia kuzibomoa nyumba hizo kwa hiari.
“Hatuna
msamaha kwa watu waliojenga katika eneo hili kwa sababu wamesababisha
tupoteze kodi nyingi, hivyo baada ya kumalizika muda huo mamlaka husika
zibomoe nyumba zote zitakazosalia.”
Awali
Waziri Mkuu alikutana na Mkuu wa wilaya ya Nakonde nchini Zambia, Bw.
Field Simwinga ambaye alisema wamekubaliana na utekelezaji wa agizo hilo
kwa kuwa jambo hilo linaathiri shughuli za mipakani kwa pande zote
mbili.
Bw.
Simwinga alisema tayari wameshaanza kuwaeleza wananchi wao waliojenga
ndani ya mpaka huo kuanza kuondoka, ambapo Waziri Mkuu amesema wanataka
eneo hilo liwe wazi ili iwe rahisi kuutazama mpaka huo kwa umakini.
Mkuu
huyo wa wilaya ya Nakonde alisema utekelezaji wa jambo utafanikiwa kwa
urahisi kutokana na ushirikiano wa Serikali za Tanzania na Zambia.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, JULAI 21, 2017
No comments:
Post a Comment