Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelote Stephen (katikati), akionyeshwa kitanda cha kujifungulia na Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk. Boniface Kasululu muda mfupi kabla ya kuvikabidhi kwa Wakuu wa Wilaya. Kutoka kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Julieth Binyura akifuatiwa na Katibu tawala wa Mkoa Bernard Makali. (Picha na Ofisi ya Mkoa).
Na Mwandishi Wetu, Rukwa
Katika kuendeleza dhana ya maendeleo hayana chama Mkuu
wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amewashirikisha madiwani wa
chama cha CHADEMA katika harambee ya ghafla iliyolenga kumalizia ujenzi wa
jengo la huduma za afya ya uzazi na mtoto katika kituo cha afya Mazwi, Manispaa
ya Sumbawanga.
Harambee hiyo ilifanyika muda mfupi kabla ya Mh.
Zelote Kukabidhi jumla ya vitanda vya kujifungulia 16, vitanda vya wagonjwa 80,
magodoro 80 pamoja na mashuka 200 kwa wakuu wa wilaya ikiwa ni sehemu ya mgawo
wa vifaa hivyo uliofanyika nchi nzima kupitia juhudi za Rais Dk. John Pombe
Magufuli katika kuimarisha huduma za uzazi nchini.
Akiongea mbele ya wananchi waliohudhuria katika tukio
hilo Mh. Zelote alisema kuwa serikali ya awamu ya tano sio ya maongezi bali
vitendo hivyo kuwataka waheshimiwa madiwani sita wakiwemo watatu wa CHADEMA wakiongozwa
na Meya wa Manispaa ya Sumbawanga kuchangia ujenzi wa jengo hilo jipya ili
kuboresha huduma kwa wananchi waliowachagua.
“Ili Manispaa iwe jiji tunahitaji huduma bora katika
kituo hiki hivyo basi, Mimi Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelote Stephen nachangia
tani tano za “cement” ambayo ni mifuko 100,” alitangulia kusema.
Harambee hiyo ilikusanya ahadi ya vifaa vyenye thamani
ya shilingi milioni 5.5 huku jengo hilo likiwa limegharimu Shilingi Milioni 16
hadi kusimama.
Awali akisomewa taarifa kabla ya kuzindua huduma ya
kujifungua iliyoanza tarehe 1/7/2017 katika kituo hicho afisa muuguzi Mariam
Kidya alieleza kuwa jengo lililopo la huduma ya afya ya uzazi na mtoto lina
uwezo wa kuhudumia kina mama 2,327 lakini kwa mwaka 2016/2017 limeweza
kuhudumia kina mama 31,257 jambo lililopelekea kuanzisha ujenzi wa jengo jipya
ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa akina mama.
Aidha Mh. Zelote aliwasisitiza wananchi kuendelea
kulipa kodi ili kuendelea kuboresha huduma na kuleta maendeleo katika sekta
mbalimbali nchini na kuonya kuwa wale watakaolipishwa ili kupata huduma ya afya
ya uzazi na mtoto basi wafike ofisini kwake ili achukue hatua.
“Ndio maana
Mheshimiwa Rais amesisitiza sana watu tulipe kodi wote ili kutatua kero
mbalimbali za wananchi hususan watu wa hali ya chini. Nataka nisisitize ulipaji wa kodi ili kazi
kama hii na zingine zifanyike.
Kwa upande wake mganga mkuu wa mkoa Dk. Boniface
kasululu alipokuwa akisoma taarifa ya huduma ya afya na uzazi ya mkoa, alisifu
uamuzi wa Rais Dk. John Pombe Magufuli wa kununua vifaa hivyo kupitia bohari
kuu ya dawa (MSD) kwani changamoto hizo zimekuwa zikiwasumbua kwa muda mrefu
kuanzia ngazi ya mkoa hadi katika halmashauri.
“Sekta ya afya kukabiliwa na changamoto kadhaa kubwa
ikiwa ni upungufu wa vifaa na vifaa tiba muhimu na ufinyu wa miundombinu ya
kutolea huduma kwa maana ya majengo, hivyo tunapongeza juhudi za rais wetu
mpendwa kutupatia vifaa hivi na tunaahidi kuvitunza ili viweze kuwasaidia kina
mama wa mkoa wetu,” Alisema.
No comments:
Post a Comment