HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 19, 2017

Ripoti ya APRM Yaingarisha Tanzania Kiutawala Bora

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, akikata utepe kama ishara ya uzinduzi rasmi wa taarifa ya tathmini ya utawala bora nchini uliofanyika jijini Dar es Salaam, jana. Kushoto ni Mjumbe wa Jopo la Watu Mashuhuri na Kiongozi wa Mchakato wa Tanzania toka APRM, Bridget Mabandla. (Picha na Eliphace Marwa, Maelezo).

Na Bushiri Matenda
 
Tanzania imetajwa kuwa moja ya nchi katika Bara la Afrika inayotekeleza kwa vitendo dhana ya utawala bora, demokrasia, amani na utulivu, hali inayochochea ustawi wa wananchi wake na katika Bara la Afrika kwa ujumla.

Akizungumza wakati akizindua ripoti ya Mpango wa Kijitathmini Kiutawala Bora Barani Afrika (APRM, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alisema kuwa ripoti hiyo imeonesha kuwa Tanzania imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kuboresha maisha ya wananchi wake hasa kwa kutoa kipaumbele katika kutoa huduma bora za afya, maji, elimu na nishati.
 
“Kwa niaba ya Serikali naahidi kuwa tutaendelea kusaidia mpango huu ili uwe endelevu na kutoa matunda yaliyokusudiwa kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, asasi zisizo za Kiserikali, wananchi na kila mmoja wetu,” alisisitiza Mhe. Samia.
 
Alieleza kuwa Tanzania inaitazama APRM kama chombo muhimu cha kusaidia kukuza demokrasia na ushiriki wa wananchi katika kutatua changamoto.
 
“Ukweli ni kwamba APRM ina akisi na kutukumbusha philisophia na maono ya Mwalimu Nyerere ya Tujisahihishe,1962 na Mwongozo wa TANU, 1975 ambazo zinazungumzia dhana ya kujikosoa na kuchukua hatua za kujirekebisha kama njia sahihi za kukabiliana na changamoto zinazolikabili taifa letu. Sasa kwetu sisi (Tanzania) APRM inatazamwa kama chombo muhimu kinachozipa uhai philosofia na maono ya Mwalimu,” alieleza.
 
Akizungumzia changamoto zilizoainishwa katika ripoti hiyo Mhe. Samia alisema kuwa kwa kuona umuhimu Serikali imeweka mkakati na kuujumuisha katika Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025 inayolenga kuleta mabadiliko na kukuza uchumi kwa kufanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati unategemea viwanda.
 
Akifafanua Mhe. Suluhu amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imejikita katika kujenga uchumi wa viwanda kwa kuhakikisha kuwepo kwa nishati ya kutosha kuchochea ukuaji wa sekta hiyo na kuwepo kwa mpango kazi unaotekelezwa kati ya mwaka 2011-2035 kwa kuzingatia mipango ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu katika kuhakikisha kuwa kuna upatikanaji wa uhakika wa nishati, kazi inayotekelezwa na Wakala wa Huduma za Umeme Vijijini (REA).
 
Aliongeza kuwa eneo jingine ni uwezeshaji wanawake kiuchumi, kielimu, kuwapa fursa wanawake kupata mikopo, huduma za afya, elimu na kuwajengea uwezo ili waweze kushiriki kikamilifu katika uzalishaji mali na kujenga uchumi kwa kuondoa changamoto zinazowakabili katika sekta ya ardhi.
 
Pia alibainisha kuwa Serikali imekuwa ikichukua hatua katika kupambana na vitendo vya rushwa na imekuwa ikiwafikisha mahakamani wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo kwa kuunda Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (TAKUKURU) na kuiimarisha ili iweze kutekeleza majukumu yake vyema.
 
Hatua nyingine ni kukabiliana na vitendo vya utakatishaji fedha, kuundwa Tume ya Maadili ya Viongozi na kuwashirikisha wadau mbalimbali katika kupambana na rushwa vikiwemo vyombo vya habari.
 
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Uendeshaji wa APRM Tanzania Prof. Hasa Mlawa amesema kuwa Tanzania imefanikiwa katika kuimarisha na kudumisha Muungano, amani na utulivu, kuimarisha ubora na upatikanaji wa huduma za jamii, usawa wa jinsia na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi.

Naye Makamu Mwenyekiti wa jopo la watu mashuhuri na kiongozi wa Mchakato wa Tanzania Mhe. Brigitte Sylivia Mabandla ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kufanikisha ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika ikiwemo Afrika Kusini na jitihada za kuimarisha ushirikiano wake na mataifa mengine.

Kutokana na Tanzania kufanya vizuri katika tathmini hiyo ya APRM ambapo ripoti ya Tanzania ilipigiwa mfano na zaidi ya marais kumi wa Afrika, Brigitte ameiomba Serikali ya Tanzania kuendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi hiyo na pia kuendelea kuchukua hatua za kutatua baadhi ya changamoto ili iendelee kuwa kinara katika masuala ya utawala bora.

Mpango wa Hiari wa Nchi za Umoja wa Afrika Kujipima kwa vigezo vya utawala bora, ulibuniwa na viongozi wa umoja huo mwaka 2003 kuziwezesha nchi wanachama kujitathmini kwa vigezo vya utawala bora katika maeneo ya Demokrasia na Utawala wa kisiasa, Usimamizi wa Uchumi, Utendaji wa Mashirika ya Biashara na Maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi.

Uzinduzi wa Ripoti hiyo ulihudhuriwa na viongozi waandamizi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mabalozi wanaowakilisha nchi zao humu nchini, wanadiplomasia na washirika wa maendeleo.

Wengine walioshiriki hafla hiyo ni Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wawakilishi asasi za kiraia, wasomi na watafiti wa masuala ya utawala bora na maendeleo, vyama vya siasa na wananchi.

No comments:

Post a Comment

Pages