Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen ameonya
vikali wale wanaoendeleza gumzo la kuwatetea wanafunzi wanaopata mimba
wakitaka warudishwe shule huku watoto wao wakiwa wanawalinda na
kuhakikisha wanafanikiwa katika maisha.
Ameyasema
hayo alipofanya ziara kujionea maandalizi ya mapokezi ya wanafunzi wa
kidato cha tano katika shule mbili za Wilaya ya Nkasi kwa muhula wa
mwaka 2017/2018, ambapo kwa Mkoa wa Rukwa wanafunzi 1,155 wamepangiwa
kujiunga na shule 13 zinazochukua wanafunzi wa kidato cha Tano.
Mkuu
wa Mkoa alisema kuwa kwa Mkoa wa Rukwa pekee kuna kesi 165 za wanafunzi
kupata mimba tangu Januari hadi Juni mwaka huu na kesi zao zinaendelea
kushughulikiwa ili kuwapata watuhumiwa na kuwachukulia hatua.
“Katika
Mkoa wangu huu adui yangu namba moja ni yule ambae anampa mtoto wa kike
mimba na yeyote anayetetea masuala yanayozunguka mimba, tusije
tukaruhusu watu ambao wameshafanikiwa na watoto wao kielimu halafu
wanakuwa kwenye majukwaa ya kuwaharibia watoto wa wazazi wengine, shule
siyo Clinic wala siyo Maternity, wanafunzi hawaji shuleni kuapata mimba
ni kusoma tu,” Mh. Zelote alisisitiza.
Sambamba
na hilo aliwataka wazazi wote kukemea vitendo hivi vinavyolenga
kukatisha ndoto za wanafunzi hawa ambao wanaandaliwa kuijenga Tanzania
ya viwanda, na kuongeza kuwa watoto ni wa watanzania si lazima awe wa
kumzaa hivyo inampasa kila mzazi kuwa na uchungu pale anapoona mtoto wa
mwenziwe amekatishwa ndoto zake kwa kupata mimba.
“Kwa
wazazi na watu wazima hili lazima tulisimamie wote, mzazi, mtu mzima
akimwona mtoto anafanya kitu kibaya achukue hatua, akemee na sio kupiga
makofi na kutetea,” Alisema.
Katika
kulisisitiza hilo Mh. Zelote aligawa nakala ya Marekebisho ya Sheria
Mbalimbali Namba 2 ya mwaka 2016 ambayo katika kifungu 60A (1 – 4)
imebainisha adhabu kwa watu wanaowapa mimba au kuoa ama kuolewa na
mwanafunzi, kwa kifungo cha miaka 30 jela.
Awali
akisoma taarifa fupi ya hali ya mimba katika Shule zilizopo Wilaya ya
Nkasi Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nkasi Abel Adam Ntupwa alisema
kuwa wananchi na wazazi wengi hawaifahamu sharia ya elimu inayotaka
mwanafunzi akipata mimba taarifa na vielelezo vinapelekwa kwa afisa
mtendaji kata au Kijiji na kesi kupelekwa polisi kisha mahakamani.
“Baadhi
ya wazazi na watendaji wanakula njama ya kutaka kumaliza kesi kienyeji
kwa wazazi wa pande mbili kupatana, hivyo uongozi wa wilaya utatoa elimu
pana juu ya haki ya msichana kusoma mpaka kumaliza na kuwachukulia
hatua wale wanaosaidia kuficha wahalifu wa mimba,” Alisema.
Katika
kuonesha umakini wa kulifuatilia suala hilo Afisa Elimu wa Mkoa wa
Rukwa Robert Nestory alisisitiza kuwa upimwaji mimba kwa wanafunzi
ufanywe mara kwa mara isiwe tu wakati shule zinapofunguliwa.
“Huu
utaratibu wa kuwapima wanafunzi wakati shule zinapofunguliwa tuuache,
upimwaji huu uwe ni wa mara kwa mara, na maafisa elimu wanapokwenda
kutembelea shule mbali mmbali basi ni jukumu lao kuonana na wazazi ili
wawape elimu ya sharia hii na sio tu kumuachia Mkuu wa Wilaya kazi
hiyo,” Aliongeza.
Wakati akimkaribisha Mkuu wa
Mkoa nae Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda alibainisha mpango wa
kuwatangaza kwenye redio watuhumiwa wote ili jamii isikie na kuondoa
dhana ya kuwaficha katika maeneo yao wanayoishi.
“Orodha
yao watuhumiwa wote tunayo na redio tunayo, Nkasi FM, tutawangaza kwa
majina ili wafamu kwamba wanatafutwa ili kuwatia hofu hasa maeneo ya
huku vijijini,” Mh. Mtanda alimalizia.
No comments:
Post a Comment