WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, Bw. Eliseyi Mgoyi pamoja na maofisa wengine watatu kwa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma.
Pia
amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa
wa Songwe, Bw. Damian Sutta kuwakamata na kuanza kuwachunguza haraka maofisa
hao na kisha ampelekee taarifa ofisini kwake.
Waziri
Mkuu amewasimamisha kazi maofisa hao leo (Jumapili, Julai 23, 2017) wakati
alipozungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi kwenye ukumbi wa
Shule ya Sekondari Vwawa, akiwa katika ziara yake ya kikazi.
Maofisa
wengine waliosimamishwa kazi ni pamoja na Mweka Hazina wa Halmashauri hiyo Bw.
Simon Noel, Bw. Bahati Chomoka ambaye ni
Cashier na Bw. Remmy Haule ambaye ni
Ofisa Ugavi.
Waziri
Mkuu amesema Maofisa hao wamekiuka sheria za matengenezo ya magari ya Serikali
kwa kwenda kutengeneza katika gereji ambazo hazikusajiliwa na wala hazifanyi
shughuli hiyo, jambo ambalo halikubaliki.
Amesema Kampuni
ya Umbwila ni moja kati ya Kampuni zinazolipwa fedha nyingi za utengenezaji wa
magari ya Halmashauri ya wilaya ya Mbozi huku ikiwa haina sifa za kufanya kazi
hiyo ya utengenezaji magari.Kampuni zingine ni Julius Diesel, Kasaba na Mtoni
Garage.
“Mfano duka
la Umbwila ambalo linauza vipuri vya
magari lakini Halmashauri inalilipa fedha kwa ajili ya utengenezaji wa magari jambo
ambalo si sahihi kwa sababu lile ni duka la vipuri na si gereji. Wanamlipa
muuza vipuri kama mtengeneza magari”
Waziri
Mkuu ameongeza kuwa “hatuwezi kuendesha Serikali kwa namna ambayo haikubaliki
kwani watu tuliowapa dhamana ndio wanaongoza kwa vitendo vya rushwa na ufisadi.
Wameifanya Halmashauri hii kama shamba la bibi.”
Kufuatia
hali hiyo, Waziri Mkuu amemtaka Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mheshimiwa Eric
Ambakisye kuhakikisha anasimamia vizuri utendaji ndani ya Halmashauri hiyo na
kwamba Serikali inataka watu waadilifu na wenye uaminifu na nidhamu.
“Halmashauri
inanuka rushwa tunataka iwe safi. Hatuwezi kukubali kuona Halmashauri hii na
zingine nchini zikigeuzwa kuwa magenge. Kwa Serikali hii no, hatuhitaji rushwa
wala harufu ya ufisadi.”
Waziri Mkuu
amesema Serikali haiwezi kuvumilia kuona watumishi waliopewa dhamana
wakijinufaisha kwa fedha za umma na kuwaacha wananchi wakiendelea kuteseka kwa
kukosa huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo za maji, afya na elimu, hivyo
itaendelea kuwachukulia hatua.
Pia Waziri
Mkuu amewataka Madiwani na Wakuu wa Idara katika Halmashauri zote nchini wabadilike
na wahakikisha wanashirikiana na kufanya kazi kwa ushirikiano kwani
wakigawanyika watashindwa kutekeleza majukumu yao ya kuwatumikia wananchi.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI,
JULAI 23, 2017
No comments:
Post a Comment