Na Benedict
Liwenga-WHUSM, Kampala
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe. Dkt.
Harrison Mwakyembe amesema kwamba, Tanzania iko tayari kuwa wenyeji wa Tamasha
la Utamaduni na Sanaa Afrika Mashariki maarufu kama JAMAFEST kwa mwaka 2019.
Kauli hiyo ameitoa jana Mjini Kampala nchini Uganda wakati wa
Ufungaji wa Tamasha hilo kwa mwaka 2017 ambapo wenyeji kwa mwaka huu walikuwa
ni nchi ya Uganda.
Mhe. Mwakyembe amezipongeza nchi Wanachama wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki (EAC) ambazo zimehudhuria tamasha hilo kwa ushirikiano wa hali
ya juu katika kubadilishana uzoefu na ujuzi juu ya masuala mbalimbali
yanayohusu utamaduni na sanaa kwakuwa yameongeza mahusiano mapya ya karibu
baina ya nchi hizo.
Waziri Mwakyembe aliezea kufurahishwa kwake kwa kujionea
ngoma mbalimbali za kitamaduni toka kwa nchi wanachama ambazo zinaakisi
uhalisia wa utamaduni wa nchi hizo, pia amefurahishwa na kwa kujionea bidhaa
mbalimbali adimu toka kwa nchi hizo jambo ambalo amesisitiza kwamba nchi
wanachama hazinabudi kuendelea kushirikiana katika kuzilinda tamaduni hizo na
kuendelea kujifunza ujuzi mbalimbali wa kazi za sanaa.
“Nilipotembelea Maonyesho ya Tamasha hili pale katika viwanja
vya Kololo nilifurahi sana kujionea ngoma za kitamaduni toka kwa vikundi
mbalimbali vya nchi wanachama wa Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki, hakika
inapendeza sana, kwakweli tuzidi kuzilinda tamaduni zetu na kushirikiana kwa
karibu zaidi”, alisema Mhe. Mwakyembe.
Akiongea kuhusu suala la Tanzania kukubali kuwa wenyeji wa
Tamasha lijalo litakalofanyika mwaka 2019, Dkt. Mwakyembe alisema kwamba,
Tanzania iko tayari kuwa wenyeji katika tamasha hilo lijalo na amezitaka nchi
wanachama kujitahidi kushiriki pasipo kukosa wakiwa na bidhaa zao za kutosha
huku akiwaahidi kuwa pindi wajapo Tanzania watafurahia mambo mengi na kujionea
namna Watanzania wanavyo chapa kazi kutokana na kaulimbiu ya ‘HAPA KAZI TU’
iliyoasisiwa na Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Dkt. John Pombe Magufuli.
“Kwakuwa mwaka 2019 ni mzunguko wa Tamasha kama hili niwaambie
kwamba, Tanzania iko tayari kuwa mwenyeji wa Tamasha hili na nawakaribisheni
kwa dhati kabisa mje kujionea nchi yetu na namna tunavyofanya kazi kwa bidii,
lakini pia mje na bidhaa nyingi zaidi kwa ajili ya kuwaonyesha Watanzania”,
alisema Dkt. Mwakyembe.
Tamasha la JAMAFEST lilianzishwa mwaka 2013 nchini Rwanda na
baadhi ya Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo kwa mwaka huu tamasha
hilo linafanyika mjini Kampala nchini Uganda ambapo kwa mwaka 2019 linatarajiwa
kufanyika nchini Tanzania.
No comments:
Post a Comment