Na Benedict
Liwenga-WHUSM.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe.
Anastazia Wambura amelipongeza Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa
ufanisi wao wa kazi huku akiwataka kufanya kazi kwa ukaribu na Serikali ya
Awamu ya Tano ili kuleta maendeleo katika soka.
Mhe. Wambura ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam wakati
alipotembelea ofisi za Shirikisho hilo ili kujua namna wanavyotekeleza majukumu
yao ikiwemo changamoto za shirikisho pamoja na maendeleo ya soka nchini.
Akiongea na Viongozi mbalimbali na wadau wa soka katika ziara
yake hiyo, amesema kwamba anaridhishwa na kazi wanazofanya TFF na amewapongeza
kwa kupata uongozi mpya wa Shirikiho hilo na kuwasisitizia kujenga mahusiano ya
karibu na wadau wa soka ikiwemo kuwajengea uwezo vijana ili kukuza vipaji vyao
na hatimaye kuleta heshima kwa Taifa.
“TFF hongereni kwa kazi kubwa na nzuri mnayoifanya, hakika
mnajitahidi sana lakini niwaombeni muzidi kushirikiana na Serikali katika
kuhakikisha kwamba tunapata maendeleo mazuri katika soka, hivyo ni vema mkawa
mnajenga mawasiliano na Viongozi wa Serikali mara kwa mara ili na sisi tupate
kujua mambo yanayofanyika”, alisema Mhe. Wambura.
Sambamba na hilo, Naibu Waziri Wambura amesisitiza juu ya
suala la ugawaji wa vifaa vya michezo ikiwemo mipira ya kuchezea katika maeneo
mbalimbali nchini huku akisema kuwa, ugawaji huo uwe wa uwiano sawa ili
pasitokee eneo moja likawa linakosa vifaa hivyo kwakuwa vijana wote ni
Watanzania na wana haki sawa ya kushiriki katika michezo.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo, Bw.
Kidao Wilfred amesema kwamba, TFF imejitahidi kuwasaida vijana mbalimbali
wakiwemo Serengeti Boys kwa kuwapatia vitendea kazi na amepokea ushauri wa
Naibu Waziri wa kuendelea kujenga uhusiano wa karibu na Serikali ili kukuza
soka nchini.
“TFF tumekuwa tukiwaandaa vijana mbalimbali ili kuweza
kuwapata wenye vipaji vizuri na tumepanga kuwa vijana hawa waweze kupatiwa
shule ambapo watakuwa wanajifunza masuala mazima ya soka na nikieleze tu
Mheshimiwakwamba ushauri wako wa kujenga ushirikiano na Serikali tumeupokea na
tunaufanyia kazi”, alisema Wilfred.
No comments:
Post a Comment