WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa mkoa wa Pwani waboreshe
miundombinu ya maeneo waliyoyatenga kwa ajili ya ujenzi wa viwanda ili
waweze kuwavutia wawekezaji wa nje na ndani.
Ametoa
agizo hilo leo (Jumanne, Septemba 19, 2017) wakati akizungumza na kwa
nyakati tofauti na wafanyakazi wa kiwanda cha kutengeneza sabuni ya unga
cha Keds kilichopo Kibaha na kiwanda cha kutengeneza vigae cha Twyford
kilichopo Chalinze.
Waziri
Mkuu amesema ameridhishwa na kasi ya maendeleo ya ujenzi wa viwanda
mkoani Pwani na amewaagiza viongozi wahakikishe maeneo yaliyotengwa kwa
ajili ya uwekezaji yanakuwa na miundombinu muhimu kama maji, umeme na
barabara.
“Nimefarijika
kuona miradi hii mikubwa ya ujenzi wa viwanda ikiwa katika hatua za
mwisho kukamilika, nawashukuru kwa kuunga mkono mkakati wa Rais Dkt.
John Magufuli wa kukuza uchumi kupitia sekta ya viwanda.”
Amesema
mbali na viwanda hivyo kutoa ajira nyingi kwa Watanzania, pia
vitakapoanza uzalishaji vitawawezesha wananchi kupata bidhaa mbalimbali
kama vigae kwa bei nafuu kwa kuwa vitakuwa vinazalishwa nchini.
Pia
Waziri Mkuu amewataka wananchi wanaofanyakazi kwenye viwanda hivyo wawe
mabalozi wazuri wa Taifa kwa kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu
mkubwa ili kuwathibitishia wawekezaji kwamba wao wanauwezo mkubwa wa
kufanya kazi na hakuna haja ya kutafuta wafanyakazi kutoka nje ya nchi.
Awali,
Mkurugenzi Mtendaji wa viwanda hivyo Bw. Jack Feng amesema ujenzi wa
huo umekamilika kwa asilimia 90 na sasa wako katika hatua za mwisho
ikiwa ni pamoja na ufungaji wa mitambo na vinatarajiwa kuanza uzalishaji
Oktoba mwaka huu.
Amesema
vigae watavyovizalisha wanatarajia kuviuza kwa gharama nafuu kwa sababu
asilimia 95 ya malighafi inapatikana ndani ya nchi. Pia ameahidi kutoa
ajira nyingi kwa wananchi waishio kwenye maeneo yanayozunguka viwanda
hivyo.
Kwa upande wake,
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarest Ndikilo amemuomba Waziri Mkuu
awasaidie upatikanaji wa nishati ya umeme ya kutosha kuweza kuendesha
viwanda katika mkoa huo.
Mhandisi
Ndikilo amesema mahitaji waliyonayo ya nishati ya umeme ni megawati 92,
ambapo kwa sasa wanasambaziwa megawati 40, hivyo ameomba suala hilo
lipatiwe ufumbuzi wa haraka ili lisije kuathiri uzalishaji.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, SEPTEMBA 19, 2017.
No comments:
Post a Comment