Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen
ameutahadharisha Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini kutorudia makosa
yaliyokuwa yanafanywa na Halmashauri kabla ya wakala huo kuanzishwa.
Amesema kuwa matumizi mabaya ya fedha za barabara pamoja na
barabara hizo kujengwa chini ya viwango na kuisababishia serikali hasara ya
kufanya matengenezo ya mara kwa mara ni miongoni mwa changamoto ambazo serikali
imeamua kuzitafutia ufumbuzi kwa kuanzisha Wakala huo.
“Ukiitwa Injinia na kazi yako iendane na cheo chako, sio
unafanya kazi mpaka hata sisi ambao hatuna ujuzi huo tukiona tunasema hii ipo
chini ya kiwango, na hapo mwanzo serikali ilikuwa inaelekeza pesa nyingi sana
kwenye barabara lakini kiuhalisia barabara hazipo na muda mwingine mvua
zinataka kuanza ndio utaona mkandarasi anaingia barabarani kwenda kutengeneza
barabara,” Mh. Zelote alifafanua.
Ameyasema hayo alipokuwa akifungua kikao cha kwanza cha bodi
ya barabara kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
Amesisitiza kuwa kwa kuimarisha sekta ya barabara vijijini ndio
miongoni mwa hatua za kuuendea uchumi wa Viwanda ambao ndio kipaumbele cha
serikali ya wamu ya tano inayoongozwa na Mh. Dk. John Pombe Magufuli.
Hivyo ametoa wito kwa wakala huo kuhakikisha wanafanya kazi
yao kwa uadilifu na kuhakikisha mabadiliko yanaonekana na kuwaasa kuacha
kufanya kazi kwa mazoea na hatimae kurudisha nyuma azma ya serikali ya awamu ya
tano.
No comments:
Post a Comment