Na Benedict Liwenga-WHUSM
Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe ameahidi kuhakikisha kwamba
suala la uharamia wa kazi za filamu za Watanzania nchini unakomeshwa mara moja kwa
kuwasaka wahusika na kuwafikisha kwenye vyombo vya Sheria.
Kauli hiyo ameitoa leo Jijini Dar
es Salaam wakati alipokutana na Wamiliki wa Majumba ya Kuonyeshea Sinema ambapo
moja ya changamoto kubwa aliyotajiwa na wamiliki hao ni suala la uharamia wa
kazi za sanaa jambo ambalo linawakwamisha wamiliki hao kutokana na ukweli
kwamba baadhi ya watu wasio waaminifu wamekuwa wakivujisha filamu mpya kwa
kuziuza kiholela mitaani na wengine wakihuisha filamu hizo katika mitandao ya
kijamii jambo linalosabibisha hasara kubwa kwa wasanii na wamiliki wa majumba
ya sinema.
Mhe. Mwakyembe amesikitishwa na
vitendo vya baadhi ya watu hao wanaojihusisha na uharamia wa kazi za filamu za
Watanzania huku akiapa kuwashughulikia popote walipo watu hao ili kuhakikisha
kuwa Wasanii wananufaika na kazi zao na pia Wamiliki wa Majengo ya Sinema
wananufaika pia kwa kuonyesha kazi za wasanii hao kwa utaratibu ambao
hautomuumiza msanii mwenye kazi yake.
“Najua baadhi ya Wamiliki wa
Majumba ya Sinema mnapata hasara, na hata baadhi ya Wasanii pia, suala hili
linanikera sana na kamwe haikubaliki hata kidogo, tutahakikisha kwamba watu wa
namna hii wanatoweka katika tasnia yetu, tutawasaka popote walipo na kuwapeleka
kwenye vyombo vya Sheria kwani Serikali hii sio ye mchezo na watu wa namna
hii”, alisema Dkt. Mwakyembe.
Ameongeza kuwa, yeye kama Waziri
mwenye dhamana na Wizara hiyo atahakikisha kwamba hamasa ya kutosha inatolewa
kwa Watanzania ili wawe na utamaduni wa kuangalia sinema zinazotengenezwa
nchini katika Majumba ya Sinema yaliyopo nchini.
Aidha, Dkt. Mwakyembe amewapongeza
Wasanii nchini kwa kutoa kazi nyingi huku akiwataka kuhakikisha kwamba ubora
unazingatiwa na maadili yanazingatiwa kwa ajili ya jamii na pia amewashauri Wamiliki
wa Majumba hayo kutenga siku maalum ambayo itakuwa ikitumika kuonyesha Sinema
za Kiswahili zenye maadili na kuzitaka sinema hizo kupewa muda wa kutangazwa katika
vyombo vya habari nchini ili wananchi wengi wapate kuzijua na kuweza kutembelea
majumba hayo kwa ajili ya kuzitazama.
“Mi nadhani na sisi Tanzania
tukianzisha utamaduni wa kwamba siku Fulani ni siku ya kuonyesha Sinema za
Kiswahili tu, hii itaweka historia nchini lakini iwe picha nzuri tu na
tuzitangaze filamu hizo na sisi kama Wizara tuna haja ya kuongea na baadhi ya
vituo vya televisheni, magazeti pamoja na redio kuzitangaza filamu hizo kwani
hii itasaidia kuinua soko la filamu nchini. Bodi ya Filamu Tanzania hakikisheni
kwamba pindi itakapoamuliwa kuwa siku fulani ni siku ya kuonyesha filamu za
Kiswahili basi muone haja ya kuzipunguzia tozo baadhi ya filamu hizo
zitakazokuwa zikionyeshwa lakini tu mpaka hapo itakapoamuriwa”, alisema Dkt.
Mwakyembe.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa
Wizara hiyo, Mhe. Juliana Shonza amewapongeza Wasanii wa Tanzania kwa kujitoa
kwao katika kuonyesha vipaji vyao katika kuhakikisha kwamba vipaji hivyo
vinaitangaza Tanzania Kimataifa.
“Nafurahi kuona kuwa Filamu za
Watanzania zinafanya vizuri na Tanzania tuna Waigizaji wanaofanya vizuri
kwahiyo naamini kwamba mkiitumia vizuri hiyo fursa ya uigizaji mtakuwa
mnaitendea haki nchini yetu na kuinua vipaji vyenu lakini pia mtakuwa
mmeitangaza Tanzania Kimataifa”, alisema Mhe. Shonza.
Mhe. Waziri Dkt. Harrison
Mwakyembe akiwa ameongozana na Naibu wake Mhe. Juliana Shonza kwa pamoja
wamekuwa wakikutana na wadau mbalimbali wa kisekta ikiwa ni sehemu ya utaratibu
waliojiwekea lengo likiwa kutambua changamoto zao na namna ya kuzitatua kwa
manufaa ya Taifa.
No comments:
Post a Comment