Mchezaji
wa timu ya Singida United, Shafik Batambuze amechaguliwa kuwa Mchezaji
Bora wa mwezi Septemba wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu
wa 2017/2018.
Batambuze
anayecheza nafasi ya ulinzi wa pembeni, alitwaa tuzo hiyo baada ya
kuwashinda wenzake wawili, Ibrahim Ajibu wa Yanga na kiungo Mohammed
Issa wa Mtibwa Sugar, alioingia nao fainali katika uchambuzi uliofanywa
Dar es Salaam.
Uchambuzi
huo kwa mujibu wa utaratibu hufanywa na kikao cha Kamati ya Tuzo ya VPL
inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutokana na
mapendekezo kutoka kwa makocha waliopo viwanja mbalimbali ambavyo ligi
hiyo inachezwa msimu huu.
Mchezaji
huyo alitoa mchango mkubwa kwa Singida United kupata pointi 10 katika
michezo minne, ambayo timu yake ilicheza kwa mwezi huo, matokeo ambayo
yaliiwezesha Singida United kutoka nafasi ya 10 katika msimamo na
kupanda hadi nafasi ya nne kwa mwezi huo wa Septemba. Singida United
ndiyo timu iliyokusanya alama nyingi kwa mwezi huo ukilinganisha na timu
nyingine 15 zinazoshiriki VPL.
Singida
United iliifunga Mbao FC mabao 2-1 Uwanja wa Jamhuri Dodoma, ikaifunga
Stand United bao 1-0 Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, iliifunga Kagera
Sugar Uwanja wa Jamhuri Dodoma na ilitoka sare ya bao 1-1 na Azam FC
uwanja huo huo. Michezo yote hiyo Batambuze alicheza dakika zote 90 kwa
kila mchezo, ambayo ni sawa na kucheza dakika 360.
Kwa
upande wa Ibrahim Ajibu alitoa mchango mkubwa kwa Yanga uliowezesha
kupata pointi nane kwa mwezi huo, baada ya kushinda michezo miwili na
kutoka sare miwili, ambapo pia Mohammed Issa aliisaidia timu yake kupata
pointi nane katika michezo minne iliyocheza mwezi huo, ikishinda miwili
na kutoka sare miwili.
Kampuni
ya Vodacom, ambao ndiyo wadhamini wa ligi hiyo ina utaratibu wa
kuwazawadia wachezaji bora wa kila mwezi, huku pia mwisho wa msimu
kukiwa na tuzo mbalimbali zinazohusu ligi hiyo, ambapo msimu wa mwaka
2016/2017 kulikuwa tuzo 16 zilitolewa kwa washindi wa kada mbalimbali.
Batambuze atazawadiwa Sh milioni moja kwa kuibuka Mchezaji Bora wa
mwezi.
TFF YATAWATOA MAKOCHA KATIKA MABENCHI
Bodi
ya Ligi (TPLB) ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, limewapiga
marufuku makocha watano wa timu za Ligi Daraja la Kwanza kukaa katika
mabenchi ya timu hizo kwa sababu ya kukosa sifa.
Makocha
hao ni Mathias Wandiba wa Pamba FC ya Mwanza, Salum Waziri wa JKT
Mgambo ya Tanga, Adam Kipatacho wa African Lyon ya Dar es Salaam, Omba
Thabit wa Mvuvumwa FC ya Kigoma na Ngelo Manjamba wa Polisi Dar.
Makocha
hao wamekuwa kwenye mabenchi ya timu wakifanya kazi kama makocha wakuu
katika mechi nne mfululizo za Ligi Daraja la Kwanza msimu wa 2017/2018
inayoendelea hivi sasa.
Kwa
mujibu wa kanuni ya 72 (3) (5) ya Ligi Daraja la Kwanza, Kocha Mkuu
anatakiwa kuwa na Leseni ya chini kuanzia daraja C ya Shirikisho la
Mpira wa Miguu Afrika (CAF) wakati Kocha Msaidizi anatakiwa kuwa na
sifa isiyopungua ngazi ya Kati cha Ukocha (Intermediate).
Tayari
Idara ya Ufundi ya TFF imefafanua wazi kuwa makocha hao hawana Leseni C
ya CAF hivyo hawastahili kukaa kwenye mabenchi ya timu zao kama makocha
wakuu.
Vitendo
vinavyofanywa na timu husika ni ukiukwaji wa kanuni, na ni matarajio ya
TFF kuwa viongozi wa timu hizo watasitisha mara moja kwa makocha hao
kukaa kwenye mabenchi ili kuepika adhabu.
TFF
tunachukua nafasi hii kuzikumbusha klabu husika kwamba kuanzia msimu
ujao 2018/2019 kuwa sifa ya Kocha Mkuu wa kila timu ya Daraja la Kwanza
ni Leseni B ya CAF.
PATASHIKA LIGI VPL, FDL, SDL WIKIENDI HII
Baada
ya kupisha wiki ya FIFA kwa mchezo wa kirafiki wa kimataifa ukihusisha
Taifa Stars ya Tanzania na Miale ya Moto kutoka Malawi iliyotoshana
nguvu ya bao 1-1, uhondo wa mashindano ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili, umerejea.
Kwa
upande wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea
wikiendi hii ambako kesho Oktoba 13, 2017 kutakuwa na mchezo mmoja tu
utakaokutanisha timu za Mbao FC na Mbeya City kwenye Uwanja wa CCM
Kirumba, Dar es Salaam.
Timu
hizo ziko katika nafasi za katikati katika msimamo wa VPL, lakini
ushindani unatarajiwa kuwa kwa timu za Simba SC, Mtibwa FC na Azam
ambazo kila moja ina pointi 11 na ziko kileleni kwa tofauti ya mabao ya
kufunga na kufungwa tu.
Katika
michezo ya Jumamosi Oktoba 14, 2017 Azam FC itakuwa mgeni wa Mwadui FC
kwenye Uwanja wa Mwadui wakati Kagera Sugar itawaalika mabingwa
watetezi, Young Africans kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Ndanda
itakuwa nyumbani kucheza na majirani zao Majimaji ya Songea kwenye
Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara wakati Singida United itasafiri
hadi Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi kucheza na wenyeji Ruvu
Shooting ya Pwani.
Majirani
wengine, Njombe Mji na Lipuli ya Iringa watacheza kwenye Uwanja wa
Sabasaba mjini Njombe ilihali michezo mingine ya Ligi hiyo ikifanyika
Jumapili Oktoba 15, ambako Simba itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar kwenye
Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam wakati Tanzania Prisons itacheza na
Stand United kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Ligi
Daraja la Kwanza (FDL) nayo itaendelea ambako kesho kutakuwa na mchezo
kati ya African Lyon na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Timu hizo ni za Kundi A.
Mechi
nyingine kwenye kundi hilo itafanyika Jumamosi ambako Ashanti United
itacheza na Mvuvumwa ya Kigoma kwenye Uwanja wa Uhuru ilihali Jumatatu
Oktoba 16, Kiluvya itacheza na Friends Rangers kwenye Uwanja wa Uhuru
huku Mgambo JKT ikishikamana na Mshikamano kwenye Uwanja wa Mkwakwani
jijini Tanga.
Kundi
B kwa mujibu wa ratiba ni kwamba kesho Ijumaa JKT Mlale itacheza na
Polisi Dar kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea huku michezo mingine
katika kundi hilo ikicheza Jumapili kwa michezo mitatu.
Siku
hiyo Mbeya Kwanza itacheza na Mawenzi Uwanja wa Mabatini ulioko
Mlandizi mkoani Pwani, Coastal na Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa
Mkwakwani jijini Tanga huku Mufindi United itacheza na KMC Uwanja wa
Samora mkoani Iringa.
Kundi
C litakuwa na mchezo mmoja siku ya Jumamosi Oktoba 14, 2017 ambako
Toto African itakipiga na Pamba kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini
Mwanza na michezo mingine mitatu itafanyika siku ya Jumapili Oktoba 15,
mwaka huu.
Michezo
ya Jumapili itakuwa ni kati ya Dodoma FC dhidi ya JKT Oljoro ya Arusha
kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma; Rhino Rangers itacheza Biashara
United wakati mchezo wa Alliance Schools na Transit Camp utachezwa
kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.
Ligi
Daraja la Pili (SDL), Jumapili Oktoba 15, 2017 Kundi A kutakuwa mchezo
kati ya Villa Squad na Abajalo FC Uwanja wa Kinesi, Dar es Salaam.
Jumamosi
kutakuwa na michezo miwili ya Kundi B ambako African Sports itacheza na
Pepsi kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga huku Arusha FC itacheza na
Kitayose kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Jumapili
Oktoba 15, 2017 katika kundi B hilo la B kutakuwa na mchezo mmoja kati
ya Madini na Kilimanjaro Heroes kwenye Uwanja wa Nyerere mkoani Arusha.
Kundi
C kutakuwa na michezo yote mitatu ya raundi ya tatu ambako Ihefu
itacheza na Green Warriors kwenye Uwanja wa Highland; Mkamba Rangers
itacheza na The Mighty Elephant kwenye Uwanja wa Mkamba huko Morogoro
ilihali Boma FC dhidi ya Burkinafaso zitacheza Uwanja wa Mwakangale,
Mbeya.
Kundi
D pia kutakuwa na mechi zote tatu Oktoba 14, 2017 ambako Nyanza
itacheza na Mashujaa kwenye Uwanja wa Nyerere; Area ‘C’ United itacheza
na Milambo Uwanja wa Jamhuri Dodoma wakati JKT Msange itacheza na
Bulyanhulu kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.
NI ZAMU YA WAAMUZI DARAJA I NA II
Baada
ya mtihani wa utimamu wa mwili kwa waamuzi wenye beji za FIFA na wale
wa Daraja la Kwanza kufanyika Agosti, 2017, sasa ni zamu ya waamuzi wa
madaraja ya Tatu na Pili.
Waamuzi
wa madaraja ya Tatu na Pili kuanzia leo Alhamisi Oktoba 12, 2017
wameanza vipimo kabla ya mitihani ya utimamu wa mwili katika vituo
viwili vya Dar es Salaam na Mwanza.
Kwa wale watakaopata matokeo mazuri, watapata fursa ya kupandisha madaraja kwa mujibu wa utaratibu.
Zoezi
hilo litajumuisha pia wale waamuzi wa Daraja la Kwanza walioshindwa
mitihani hiyo mwezi Agosti, mwaka huu. Hivyo nao wanaruhusiwa kwenda
kufanya mitihani tena.
Kituo
cha Dar es Salaam kitakuwa na waamuzi wa mikoa ya Dar es Salaam
yenyewe, Pwani, Morogoro, Tanga, Kilimanjaro, Lindi, Mtwara, Ruvuma,
Njombe, Iringa, Mbeya, Rukwa na Songwe.
Kituo
cha Mwanza kitakuwa na waamuzi wa mikoa ya Mwanza yenyewe, Mara,
Kagera, Simiyu, Geita, Kigoma, Arusha, Shinyanga, Tabora, Dodoma,
Singida, Manyara na Katavi.
Waamuzi
wote waende kwenye vituo vyao walivyopangiwa kama ilivyoelekezwa Oktoba
12, 2017 - ni siku ya kupima afya kabla ya kuanza kwa mitihani mingine
ukiwamo wa utimamu wa mwili hapo kesho.
……….…………………………………………………………………… ………………..………………………………..
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA
No comments:
Post a Comment