Daktari wa macho
akimfanyia uchunguzi wa macho mmoja kati ya wagonjwa waliojitokeza katika
maadhimisho ya Siku ya Afya ya Macho Mkoani Singida. (Picha na Ofisi ya Ras Singida).
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Rehema Nchimbi amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa kuanzisha operesheni maalumu ya kuwapima macho wakazi wote Mkoani hapa hususani watumishi wa serikali.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Rehema Nchimbi amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa kuanzisha operesheni maalumu ya kuwapima macho wakazi wote Mkoani hapa hususani watumishi wa serikali.
Dkt Nchimbi ametoa agizo
hilo mapema jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Afya ya Macho Duniani ambapo
asilimia 94 ya watu wenye upofu Mkoani Singida wanasumbuliwa na matatizo ya
macho ambayo yanazuilika.
Amesema ili watumishi
wa umma waweze kutoa huduma iliyo bora wanatakiwa kuwa na uoni mzuri hivyo
kuwapima ni hatua kubwa itakayosaidia kutibu na kuzuia upofu mapema.
“Mganga Mkuu wa Mkoa
sasa tunataka uanzishe operesheni tupimwe wote macho, inasikitisha kusikia hao
wote waliopata upofu takribani watu elfu 25 wangeweza kupona endapo
wangegundulika mapema kwakuwa matatizo yaliyowasababishia upofu yanazuilika”,
amesema Dkt Nchimbi na kusisitiza kuwa,
“Halmashauri zote
tengeni bajeti za kununua dawa za macho pamoja na kuhakikisha wananchi wenu
wote wanapimwa macho ili magonjwa yanayozuilika yapewe matibabu mapema,
watendaji msione fahari kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa macho wakati
mngeweza kuwasiadia”, ameeleza Dkt Nchimbi.
Awali, Dkt Nchimbi
amepokea kifaa cha kisasa aina ya Auto Perimeter Glautefield Lite kutoka kwa
Shirika la Sight Saver, chenye uwezo wa kuona taswira na matatizo ya macho
vizuri, ambacho kwa nchi nzima kinapatikana mkoani Singida peke yake.
Amesema kifaa hicho
kitawasaidi madaktari bingwa wa macho Mkoani hapa kutoa huduma bora huku
akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili wapatiwe huduma kwani uwepo wa
kifaa hicho bila kutumika kitakuwa hakina manufaa.
Dkt Nchimbi ameongeza
kuwa, kutokunywa maji ya kutosha husababisha uoni hafifu ambao hupelekea upofu
unaozuilika, hivyo amelishauri shirika la Sight Savers kuweka mpango wa
kuboresha upatikanaji wa maji na kufanya utafiti hasa maofisini endapo
watumishi wanakunywa maji ya kutosha kwakuwa yanasaidia kuzuia upofu.
Kwa upande wake
Meneja Mipango na Uendeshaji wa Shirika la Sight Savers Nchini Mhandisi Koronel
Kema amesema shirika hilo limeanzisha mradi wa kuboresha huduma za macho mkoani
Singida utakaogharimu shilingi bilioni 2.8, mradi utakaodumu kwa muda wa miaka minne.
Kema amesema mradi huo
utafadhili ujenzi wa kliniki za macho katika halmashauri za Iramba, Manyoni na
Halmashauri ya Wilaya ya Singida na kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya ili
waweze kutumia vifaa vyenye thamani ya milioni 300 ambavyo vimetolewa na
shirika hilo.
Ameongeza kuwa Mkoa
wa Singida umeongezewa mradi mwingine utakao anza mapema mwakani na kuhusisha
upimaji wa wananfunzi wote na walimu wao mashuleni ili kuweza kutibu na kuzuia
upofu katika hatua za awali.
Mmoja wa wagonjwa
Said Mwiru aliyefanyiwa upasuaji katika jicho lake kwenye maadhimisho hayo
amemueleza Mkuu wa Mkoa kuwa kabla ya upasuaji huo hakuweza kuona chochote ila
siku moja baada ya matibabu hayo anaweza kuona vizuri.
Naye Mganga Mkuu wa
Mkoa wa Singida Dkt Salum Manyatta amesema ataongeza kasi katika kutekeleza
agizo la mkuu wa Mkoa kwakuwa walikua tayari wameshaanza kuwapima watumishi
katika baadhi ya halmashauri.
Manyatta amesema
zoezi lililofanyika la upimaji watumishi katika halmashauri ya Wilaya ya
Manyoni limebainisha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya watumishi hao walikuwa na
matatizo ya macho ambayo yangepelekea upofu.
Katika kuadhimisha
siku ya afya ya macho duniani, shirika la Sight Savers limeendesha zoezi la
upimaji wa macho kwa watu 200 Mkoani hapa ambapo 84 kati yao wamegundulika kuwa
na tatizo la macho linalosababisha wapoteze uwezo wa kuona, huku Kauli mbiu ya
maadhimisho hayo ikiwa ni ‘Afya ya Macho kwa wote’.
No comments:
Post a Comment