Na Tiganya Vincent, RS –TABORA
SERIKALI ya Mkoa wa Tabora imeziagiza Halmashauri zote zenye
wafugaji wa ng’ombe kuandaa mipango ya
kuwahamasisha wafugaji juu ya ufugaji bora kwa kuwa na mifugo michache ambayo
inahudumiwa vizuri na inakuwa na tija.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey
Mwanri wakati wa mkutano uliwahusisha Wakuu wa Wilaya , Wakurugenzi
Watendaji , Wakuu wa Idara na
Seketarieti ya Mkoa wa Tabora.
Alisema kuwa wakati umefikiwa wa kuwasaidia wafugaji kuwa na
ng’ombe wa kisasa ambao wanazalisha nyama na maziwa ya kutosha kinyume na
walivyo ng’ombe wa sasa hivi ambao uzalisha wastani wa kilo 150 hadi 200 kama
ni mkubwa.
Mwanri alisema kuwa ufugaji huo wa kizamani hauwezi kumsaidia
mfugaji kusonga mbele bali utamfanya aendelee kuwa na mawazo ya kudhani kuwa na
ng’ombe wengi wasio na uzito ni utajiri.
“Natarajia Wakurugenzi Watendaji hasa wa maeneo yenye mifugo
mingi kama vile Nzega na Igunga mwende mkawaelimishe wafugaji juu ya ufugaji
bora na wa kisasa unaweza kuwasaidia kuongeza uzito wa ng’ombe na wingi wa
maziwa…wakati sisi ng’ombe wetu wanauzito wa kilo 150 wenzetu Botswana ng’ombe
anafika hadi kilo 1,000” alisema Mkuu huyo Mkoa.
Alisema kuwa sanjari na hilo ni vema idadi ya ng’ombe katika
maeneo yao ikajulikana ikiwa ni pamoja na kujua hao wanapata wapi malisho na
wawekewe alama kwa ajili ya kutenga maeneo kwa ajili ya malisho ya wanyama hao.
Mwanri alisema kuwa kutokuwa na mipango mizuri ndio maana
unakuta ng’ombe wamerundikana sehemu moja huku wakiwa hawana hata majani ya
kula mwishowe wanakufa kwa sababu ya njaa na kukosa maji.
Alisema kuwa kuanzia sasa kila Halmashauri lazima impe na
mikakati yake ya kusimamia sekta ya mifugo kwa ajili ya kuhakikisha kuwa
wafugaji wananufaika na mifugo yao na kutoa mchango katika ujenzi wa uchumi wa
viwanda ambao nchi imeazimia kuujenga.
No comments:
Post a Comment