HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 11, 2017

DC IGUNGA HAITIMISHA ZOEZI LA KUPOKEA MBEGU BORA KUTOKA COSTECH-OFAB

 Wakulima wa Kijiji cha Igogo wanaunda Kikundi cha Imala Makoye katika Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora wakiwa wameshika mbegu ya mahindi ya Wema 2109 baada ya kukabidhiwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB) katika uzinduzi wa shamba darasa uliofanyika jana wilayani huo. Mgeni Rasmi katika uzinduzi huo alikuwa mkuu wa wilaya hiyo, John Mwaipopo.
 Kaimu Ofisa Kilimo wa wilaya hiyo, Athumani Mgunya akizungumza kabla ya uzinduzi huo.
 Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi wa COSTECH ambaye ni Ofisa Mwandamizi wa COSTECH, Audax Mutagwa, akizungumza katika uzinduzi huo.
 Mkuu wa Wilaya ya Igunga, John Mwaipopo akizungumza na wakulima wa Kijiji cha Igogo wakati wa uzinduzi wa shamba darasa la mbegu ya mahindi. Kulia ni Ofisa Ugani wa Kata ya Nanga, Ambele Mwangomo.
 Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi wa COSTECH ambaye ni Ofisa Mwandamizi wa COSTECH, Audax Mutagwa, akimkabidhi mbegu ya mahindi mkuu huyo wa wilaya ya Igunga.
 Mtafiti Dk. Betrice Lyimo, akishiriki kuandaa shamba darasa la Viazi Lishe katika Kijiji cha Mwanzugi kilichopo Kata ya Igunga. Kulia ni mkulima Solo Sai wa kijiji hicho na Mwanahabari Calvin Gwabara kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha SUA mkoani Morogoro.

Na Dotto Mwaibale, Igunga Tabora

MKUU wa Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, John Mwaipopo amehitimisha zoezi la ugawaji wa mbegu bora katika mikoa ya Kagera, Geita na Tabora kwa kuipongeza Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kuwapelekea mbegu bora za mihogo, mahindi na Viazi lishe wilayani humo kwa kushirikiana na Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB)

Pongezi hizo alizitoa jana wakati akizungumza na wakulima wa Kijiji cha Igogo kilichopo Kata ya Nanga katika uzinduzi na kukabidhiwa mbegu hizo kwa ajili ya mashamba darasa kwa wakulima wa vijiji vinne vya Igogo, Mwanzugi, Sungwizi na Busomeke.

Alisema changamoto kubwa waliyokuwa nayo wakulima katika Halmshauri hiyo ni kukosekana kwa mbegu bora za mihogo na mahindi jambo liliofanya uzalishaji wa mazao kuwa mdogo.

Mwaipopo alisema kuletewa kwa mbegu hizo kutaongeza mori wa kilimo kwa wakulima wa wilaya hiyo na kuondokana na ukosefu wa chakula badala ya kutegemea zaidi zao moja la mpunga.

Alisema kazi kubwa ya serikali ni kuhakikisha inasimamia utekelezaji wa mradi huo kwa nguvu zote ili kazi kubwa iliyofanywa na watafiti kutoka Vituo vya Ukiliguru Mwanza, Maruku mkoani Tabora na Ilonga mkoani Morogoro isipotee bure.

Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi wa COSTECH ambaye ni Ofisa Mwandamizi wa COSTECH, Audax Mutagwa, alisema mbegu hizo ya mihogo aina ya Mkombozi imefanyiwa utafiti na kuonekana ina uwezo mkubwa wa kustahimili magonjwa kama ya batobato kali na michirizi ya kahawia ambayo imekuwa ikiwapatia hasara kubwa wakulima na ya mahindi ikistahimili hali ya ukame na kutoa mazao mengi.

Mutagwa aliwaomba wakulima hao kuyatunza mashamba hayo ambayo yamegharimu fedha nyingi hadi kukamilika kwake hivyo wayaendeleze kwa ajili ya kuja kutoa matunda kwa wakulima wa wilaya hiyo na kupata chakula cha kutosha na ziada kuuza.

Akieleza lengo la COSTECH na OFAB kuendesha program hiyo ya kugawa mbegu katika mikoa ya Kagera, Geita na Tabora, Mtafiti kutoka OFAB, Dk. Beatrice Lyimo alisema kuwa kazi ya COSTECH ni kuhakikisha matunda ya kazi nzuri za tafiti yanawafikia wakulima na wananchi wengine kwenye Nyanja mbalimbali hivyo hii ni moja ya utekelezaji wa majukumu ya tume hiyo.

Alisema kwa miaka mingi tafiti mbalimbali nzuri zimekuwa zikifanywa na watafiti hapa nchini lakini haziwafikii walengwa akitolea mfano wakulima,lakini COSTECH ikatafuta fedha na kuitoa tafiti hiyo kwenye vituo vya utafiti na kuwapelekea wakulima ili kusaidia kutatua changamoto ambazo zinawakabili kwenye kilimo chao.

Ofisa Kilimo kutoka Ofisi ya Mkoa wa Tabora, Said Babu akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukamilika kwa zoezi la ugawaji wa mbegu bora za mazao hayo kwenye wilaya tano za mkoa huo ambazo ni Urambo, Sikonge, Uyui, Nzega na Igunga alisema mbegu hizo zitatoa faraja na uzalishaji mkubwa wa mazao kwa wakulima.

Alisema kuwa wakazi wa mkoa huo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kupata chakula kidogo kutokana na kutegemea mazao ya chakula mihogo na viazi vitamu lakini kwa kupata mbegu hizo watapata mazao mengi.

Alisema kuwa upatikanaji wa mbegu bora hizo kutawasaidia wananchi kupata chakula cha kutosha na lishe bora kutoka kwenye viazi lishe na akachukua fursa hiyo kuishukuru  Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia COSTECH na Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo OFAB kwa kuwapelekea mbegu hizo.


Alitaja mbegu walizopata kutoka COSTECH na OFAB kuwa ni pingiri za mihogo 38,000, mbegu za viazi lishe 75,000 na mahindi kilogramu 50.

Alisema jumla ya vikundi 26 na wakulima 557 wa mkoa huo wamenufaika na mradi huo na kuwa mkoa umeamua kuanzisha kilimo cha mazao mengine ya biashara ya korosho na alizeti ili yawe mbadala wa zao la tumbaku ambalo limekuwa likiharibu mazingira.

Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kushiriana na  Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB), waligawa mbegu za migomba, viazi lishe, mihogo, na mahindi katika Mikoa ya Kagera, Geita na Tabora ili kuinua kilimo na uzalishaji wa mazao ya chakula ambapo zoezi hilo lilifikia tamani jana wilayani Igunga mkoani Tabora.

No comments:

Post a Comment

Pages