HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 20, 2017

MAVUNDE: WATU WAKIKOSA MAADILI TAIFA LINAKUFA

*Ataka vijana waweke malengo maishani mwao

NAIBU WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana), Bw. Anthony Mavunde amesema Taifa lenye maadili ndilo linaloishi na watu wanapokosa maadili Taifa linakufa.

Ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati akiwahutubia vijana zaidi 3,500 wanaosoma vyuo vya elimu ya juu vya mkoa wa Dodoma ambao walishiriki mkesha wa kusifu na kuabudu (Campus Night 2017) kwenye ukumbi wa Chimwaga, mjini Dodoma.

“Naendelea kuiona Tanzania yenye ustawi mkubwa sana kama tutakuwa na vijana wenye kumjua Mungu, wenye hofu ya Mungu na wenye kufuata maadili mema kwani kukosa maadili kunaua Taifa,” alisema Naibu Waziri huyo ambaye alikuwa mgeni rasmi.

Aliwataka vijana hao watambue kuwa wameletwa vyuoni kusoma na siyo kujihusisha na mambo ambayo ni kinyume na maadili. “Katika maisha lazima utambue njia yako, usipoijua utapata shida tu. Ukiifahamu njia yako ni lazima unaitunza hadi ikufikishe mwisho,” aliongeza.

Akitoa mfano, Naibu Waziri Mavunde aliwaeleza wanavyuo kwamba hakuna jambo baya kama mtu kufikia hatua ya kuingia chuo kikuu au chuo kingine cha elimu ya juu lakini asijue anapaswa kufanya nini.

“Hakuna jambo baya kama hivi sasa uko chuo kikuu lakini hujajua unataka kufanya nini maishani mwako. Ni sawa na kufanya biashara ya kununua mablanketi na kwenda kuyauza Dar es Salaam ambako kuna joto wakati wote au kuamua kufanya biashara ya ice cream katika maeneo ya baridi kama vile Mafinga,” alisema.

Mapema, akimkaribisha mgeni rasmi kuzungumza na wanafunzi hao, Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) ICC Dodoma, Dk. Gerald Ole Nguyaine alisema hatma ya Taifa la Tanzania iko mikononi mwa vijana na ndiyo maana wazazi, walimu na jamii wanawekeza kwenye maisha yao.

Aliwaeleza vijana hao umuhimu wa wao kutambua kusudi la Mungu kwenye maisha yao. “Na sisi tunaamini bila uwepo wa Mungu, hamtaweza kuifikia hiyo hatma mkiwa salama. Kuna kusudi aliloliweka Mungu katika maisha yako wewe ambaye ni kijana, na kamwe usikubali kwenda kaburini kabla hujatimiza hilo kusudi,” alisema. 

“Mungu ana makusudi na maisha yako na sisi ndiyo maana tunawekeza kwenye maisha yako kwa sababu tunajua lipo kusudi maalum la Mungu kukuleta duniani. Tunatumia muda wetu, na rasilmali za Taifa ili kuhakikisha tunawaonyesha njia iwapasayo. Hakuna jambo litafanikiwa maishani mwako kama hauna mahusiano mazuri na Mungu wako,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CAMPUS NIGHT DODOMA, Bw. Ibrahim Kisungwe alisema mwaka huu wamefanya tamasha la campus night kwa mwaka wa saba mfululizo na kila mwaka kumekuwa na mafanikio ya aina tofauti.

Alisema kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘Made Complete’ yaani umekamilishwa ambayo inaendana na namba saba ambayo ni namba ya ukamilifu.

Wakati huo huo, mhubiri aliyehudumu katika tamasha hilo, Mchg. Pascal Mande wa kanisa la TAG Msasani aliwaeleza vijana hao kwamba wanapaswa kujitambua wao ni akina nani na wapo vyuoni kwa kusudi gani ndipo waweze kufikia kusudi la uwepo wao.

“Kama huwezi kujitambua wewe ni nani, hauwezi kutimiza kusudi la Mungu. Hauwezi kutembea kwenye maono ya Mungu kama hajakubali kukamilishwa na Bwana Yesu,” alisema.

Tamasha hilo lilipambwa na waimbaji mbalimbali wakiwemo Mass Choir (Dodoma), Worship Experience (Dodoma), Angel Benard (Arusha), New Life Band (Arusha), Enos Lazaro (Dar es Salaam) na waimbaji wengine wadogo kama Sakina Naftari (Moshi) na Jerome Venance (Arusha).

IMETOLEWA:
JUMATATU, NOVEMBA 20, 2017 
DODOMA.
004739   Mchg. Pascal Mande wa Kanisa la TAG Msasani akihubiri wakati wa tamasha la Mkesha (Campus Night 2017) wa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu kutoka mkoa wa Dodoma lilifanyika kwenye ukumbi wa Chimwaga, UDOM, mwishoni mwa wiki. (Picha na Irene Bwire).
Mwanamuziki wa nyimbo za injili, Angel Benard na waimbaji wake, wakitumbuiza wakati wa tamasha la Mkesha (Campus Night 2017) wa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu kutoka mkoa wa Dodoma lililofanyika kwenye ukumbi wa Chimwaga, UDOM, mwishoni mwa wiki.
 Wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu kutoka mkoa wa Dodoma wakifuatilia burudani wakati wa tamasha la Mkesha (Campus Night 2017) lililofanyika kwenye ukumbi wa Chimwaga, UDOM, mwishoni mwa wiki. 

No comments:

Post a Comment

Pages