Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amezihimiza
Halmashauri zote Mkoani humo kuhakikisha zinaongeza idadi ya mashine za EFD ili
kuongeza ukusanyaji wa mapato yao katika halmashauri.
Amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri ya
Wilaya ya Sumbawanga ilikisia kukusanya Shilingi bilioni 2.3 ambapo hadi sasa
Wilaya imekusanya Shilingi bilioni 1.9 ikiwa ni ongezeko la asilimia 97 katika
makusanyo ya ndani ya Halmashauri hiyo.
“Halmashauri Ziongeze hizo mashine, kama mnavyofahamu
serikali hii inahimiza ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kutumia mfumo wa
Kielektroniki, wenyewe mmekuwa mashuhuda mmevuka kile kiwango mlichojiwekea na
kupata ongezeko la asilimi 97 kama mlivyosoma kwenye taarifa yenu, mkiongeza
mashine hizo zikafikia idadi inayotakiwa makusanyo ya ndani yatakuwa mengi
zaidi,” Alieleza.
Ameongeza kuwa makusanyo ya ndani yakiwa mengi zaidi
itasababisha shughuli za kimaendeleo kufanyika kwa wingi zaidi, ikiwemo ujenzi
wa vyumba vya madarasa, huku upungufu wa vyumba hivyo ukiwa ni 1399.
Ameyasema hayo baada ya kusomewa taarifa ya Halmashauri ya
Wilaya ya Sumbawanga katika Ziara yake ya siku mbili yenye lengo la kutembelea
miradi mbalimbali, kujitambulisha kwa watumishi pamoja na kuongea na makundi
mbalimbali ya wananchi katika halmashauri hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa H/W ya Sumbawanga
John Msemakweli amesema kuwa hadi sasa Halmashauri ina mashine za Kielektroniki
64 na uhitaji ni mashine 114 na kusababisha upungufu wa mashine 50 huku
akiahidi kuzikamilisha ili kuweza kuongeza mapato ya Halmashauri hiyo.
“Tuna upungufu wa vyumba vya madarasa 1399 na hadi sasa kwa
mpango wa kujenga vyumba vitatu kwa kila shule tuna vyumba 98 ambavyo vipo
usawa wa linta na kwengine tunaendelea kuwahamasisha wananchi kuweza kuchangia
katika ujenzi,” Alisema.
Naye Mh. Wangabo aliwaagiza kuangalia upya mpango wao wa
ujenzi wa madarasa hayo kwani itawachukua muda mrefu ikiwa watajenga madarasa
98 kwa mwaka.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akitoa
maelekezo kwa Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kuzidisha
juhudi za kukusanya mapato.
IMETOLEWA NA
OFISI YA MKUU WA MKOA WA RUKWA
No comments:
Post a Comment