NA JANETH JOVIN
UTAFITI wa mwaka
2014 uliofanywa na baadhi ya wataalamu wa masuala ya uvuvi umeonyesha kuwa licha ya Tanzania kuwa na
eneo kubwa la bahari, asilimia 90 ya wavuvi wake wamekuwa wakivua samaki tani 52,000
tu kwa mwaka tofauti na nchi zingine zenye eneo dogo lakini wanavua zaidi ya
kiwango hicho.
Akizungumzia utafiti
huo hivi karibuni wakati akitoa mafunzo
kwa waandishi wa Habari juu ya uharibifu wa mazingira kwenye bahari, Mhadhiri
wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM) kutoka Idara ya Sayansi za Maji na
Uvuvi, Dk Benaisha Benno alisema utafiti huo umebainisha kuwa hali hiyo
inachangiwa na wavuvi kutumia zana duni ambazo haziwezi kufika katika kina
kirefu cha bahari kunapopatikana samaki wengi .
Benno alisema kutokana na kuwepo kwa uhaba wa vitendea kazi
kwa wavuvi hao kumepelekea wanavua samaki wachache zaidi na kushindwa kwenda
kwenye kina hicho kirefu cha bahari.
“Tungekuwa na zana kubwa na za kisasa tungeweza kufika
katika kina kirefu na kupata samaki wengi zaidi ya hao tunaowapata sasa lakini vifaa vinavyotumiwa na wavuvi wetu vinawafanya wanashindwa kwenda kuvua samaki
katika bahari kuu matokeo yake wanashindwa kuvua samaki wakubwa na
wengi.
"Samaki wanaovuliwa na wavuvi wetu ni wadogo na uvuliwa
sehemu za karibu karibu na sio Kwenye kina cha bahari ambapo ndio upatikana samaki
wakubwa zaidi," alisema Dk.Benno
Aidha Dk. Benno aliwataka wavuvi kuacha uvuvi haramu kwani
unasababisha uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake Mtafiti Mwandamizi wa Taasisi ya Utafiti wa
Uvuvi Tanzania (Tafiri), Baraka Kuguru alisema sekta ya uvuvi ikipewa kipaumbele
itachangia ukuaji wa uchumi na hivyo kutekeleza malengo ya viwanda na uchumi wa
kati.
Kuguru alisema tafiti ziaonyesha kuwa sekta ya uvuvi
imekuwa na mchango mkubwa kwa nchi ambazo zimewekeza hasa katika ukanda wa
bahari ambapo rasilimali zilizopo kwenye bahari zina thamani ya dola za
Marekani 333 bilioni huku uwekezaji ukiwa asilimia 20 mpaka sasa.
Naye Mmoja wa wavuvi wa soko kuu la samaki la Zanzibar, Habibu
Othuman alisema wavuvi wengi hawana
sehemu rasmi ya kupata mikopo hivyo anaiomba serikali iwatengenezee mazingira
bora yatakayowawezesha kupata mikopo iliyokuwa na na riba nafuu au isiyo nariba
kabisaa.
Aidha alisema miongoni mwa changamoto inayowakabili ni ya
ukosefu wa boti zenye uwezo wa kuvua samai katika kina kirefu hivyo wanaiomba
serikali pia iingie ubia na kampuni kubwa ziweze kutafuta vyombo hivyo vya
uvuvi vinavyoweza kufika mbali.
“Serikali iingie ubia na wawekezaji wakubwa watuletee vyombo hivyo vya kisasa kisha watukopeshe
tuone kama tutashindwa kuvua samaki wengi lakini pia tunaziomba benki zije
kutupa elimu juu ya umuhimu wa kukopa kwa lengo la kukuza biashara,” alisema.
No comments:
Post a Comment