WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amepokea vifaa vya michezo vyenye thamani ya sh. milioni 50 kwa ajili ya
kuanzisha mashindano ya mpira wa miguu kwa majimbo ya mkoa wa Dar es Salaam.
Vifaa hivyo vimetolewa na
Muwakilishi wa Jimbo la Uzini, Mohammed Raza na Muwakilishi wa kuteuliwa
Bw.Ahmada Yahya Abdulwakili, ambapo mara baada ya kupokea vifaa hivyo
alivikabidhi kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Paul Makonda.
Amepokea vifaa hivyo jijini
Dar es Salaam leo
(Jumanne, Novemba 28, 2017), mashindano hayo yatakayoratibiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM)
yatahusisha vijana kutoka majimbo yote 10 ya mkoa wa Dar es Salaam.
Waziri Mkuu amewapongeza Bw.
Raza na Bw. Ahmada kwa kuona umuhimu wa vijana kushiriki katika michezo na
kuamua kudhamini mashindano hayo, ambapo mshindi wa kwanza atapata zawadi ya
gari aina ya Carry lenye thamani ya sh. milioni saba.
Amesema mashindano hayo
yatawawezesha vijana kupata fursa ya kuonyesha na kukuza vipaji vyao na
kusisitiza kwamba michezo ni muhimu kwani ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya
uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 na pia inakuza ajira, hivyo ameagiza
mashindano hayo yasimamiwe kikamilifu kwa kufuata sheria za Shirikisho la Soka
Duniani (FIFA).
Akizungumza baada ya
kukabidhi vifaa hivyo, Bw. Raza amesema sababu ya kudhamini mashindano hayo
upande wa Zanzibar na Tanzania Bara ni kumuunga mkono Rais Dkt John Magufuli
katika utekelezaji wa ilani.
Amesema mashindano kama hayo
yalifanyika kwa mafanikio makubwa Zanzibar ambapo Raza na wanaCCM wenzake
waliyadhamini. Hivyo ametoa wito kwa wafanyabiashara kudhamini mashindano kama
hayo ili kuwawezesha vijana kukuza vipaji vyao.
Kwa upande wake Bw. Makonda alimuahakikishia
Waziri Mkuu kwamba watayasimamia kikamilifu mashindayo kwa sababu ni chachu ya
kukuza vipaji vya mpira wa miguu mkoani Dar es Salaam.
Pia alimueleza Waziri Mkuu
dhamira ya mkoa huo ya kuanzisha kituo cha muziki “Music hub” ili kuwawezesha vijana wenye vipaji vya muziki jijini
Dar es salaam, kupata fursa ya kuendeleza vipaji vyao.
Mashindano ya majimbo
Zanzibar yalizinduliwa Machi 23, 2017 na Rais wa Zanzibar Dkt. Mohammed Shein
na kufungwa Novemba 25, 2017 na Waziri Mkuu, ambapo mshindi wa kwanza alipewa
zawadi ya gari aina ya Carry lenye thamani ya shilingi milioni saba.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMANNE, NOVEMBA 28, 2017.
No comments:
Post a Comment