WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameungana na wanafamilia, wananchi wa Songea katika kuomboleza kifo cha
aliyekuwa mbunge wa jimbo la Songea, Bw. Leonidas Gama, nyumbani kwa marehemu
Likuyu wilayani Songea.
Bw. Gama amefariki dunia jana (Ijumaa, Novemba 24, 2017)
katika Hospitali ya Peramiho mkoani Ruvuma alikokuwa akipatiwa matibabu. Marehemu
anatarajiwa kuzikwa Jumatatu, Novemba 27, 2017 katika kijiji cha Likuyu
wilayani Songea.
Akizungumza kwa niaba ya Serikali, Waziri Mkuu amesema kifo hicho ni
pigo kwa Serikali kwa sababu marehemu alishirikiana nayo vizuri tangu akiwa
mtumishi wa umma na hata baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa Jimbo la Songea.
Waziri Mkuu amesema msiba huo umeleta mtikisiko mkubwa kwa sababu baada
ya kurudi nchini kutoka India alikokuwa akipatiwa matibabu aliwaeleza kuwa hali
yake kwa sasa ni nzuri. ”Ametuachia pengo kubwa ambalo hatuna namna ya
kuliziba.”
Ameongeza kuwa alipokea taarifa za msiba huo kwa huzuni na mshtuko
mkubwa kwa sababu siku mbili kabla ya Waziri Mkuu kuanza ziara yake mkoani
Ruvuma, Bw. Gama alimpigia simu na kumjulisha kwamba yeye anatangulia Songea kumpokea.
“Kifo ni mipango ya Mwenyezi Mungu na kwamba Bw. Gama ametangulia nasi
tutafuata, hivyo wajibu wetu sote ni kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ailaze roho
yake mahali pema. Gama alikuwa kiongozi na mwanga wa maendeleo.”
Pia Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaomba wanafamilia, mke wa
marehemu na watoto na wananchi wa jimbo la Songea waendelee kuwa watulivu na
wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wetu.”
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Bibi Christine Mndeme
alimshukuru Waziri Mkuu kwa kutenga muda wake na kwenda kuwafariji wafiwa licha
ya majukumu mengi na makubwa aliyonayo.
Awali msemaji wa familia Bw. Issa Fusi alimshukuru Waziri Mkuu pamoja
na viomgozi mbalimbali waliojitokeza na kuwafariji baada ya kutokea kwa msiba
huo.”Kaka yetu tulimpenda sana kazi ya Mungu haina makosa.”
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, NOVEMBA 25, 2017.
No comments:
Post a Comment