HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 07, 2017

SERIKALI KUTATUA CHANGAMOTO ZA KODI ZINAZOIKABILI SEKTA BINAFSI

Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Charles Kichere, akijibu baadhi ya hoja zilizowasilishwa na Sekta Binafsi wakati wa mkutano kati ya Serikali na Sekta hiyo, uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango mjini Dodoma
 Baadhi ya wafanyabiashara na wawekezaji  kutoka sekta binafsi nchini  wakifuatilia kwa makini mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa kwenye  mkutano kati ya Serikali na Sekta  hiyo kupitia Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) kuhusu masuala ya kodi, mjini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (Mb) , akitolea ufafanuzi masuala kadhaa yanayohusu changamoto za kodi katika Sekta Binafsi wakati wa mkutano kati ya Serikali na Sekta hiyo, uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango mjini Dodoma
 
Benny Mwaipaja, Dodoma

WAZIRI wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango amewaahidi wafanyabiashara na wawekezaji nchini kwamba serikali italifanyiakazi suala la kodi katika Bajeti ijayo ya mwaka 2018/2019 ili kuboresha zaidi mazingira ya uwekezaji na biashara kupitia sekta binafsi.

Dokta Mpango ameyasema hayo mjini Dodoma katika mkutano wa tatu kati ya Serikali na Sekta binafsi ambapo masuala mbalimbali yanayohusu kodi yamejadiliwa ikiwa ni mwendelezo wa Serikali kutaka kuiimarisha Sekta hiyo ili iweze kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Alisema kuwa Serikali imedhamiria kupunguza ama kuondoa kabisa kero zinazoikabili sekta binafsi ikiwemo malalamiko ya muda mrefu ya utitiri wa kodi ili sekta hiyo iweze kuwa na nguvu na kushiriki kikamilifu katika kujenga uchumi wa viwanda utakaokuza pato la taifa na ajira nchini.

Alisema Serikali inatambua kwamba sekta binafsi ndiyo nguzo ya ukuaji wa uchumi wa Taifa ndio maana inajitahidi kupata maoni ya wadau kuhusu namna ya kuboresha mazingira yao ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini ili kuharakisha maendeleo ya nchi.

“Ni lazima dukuduku za sekta binafsi tuzisikilize, tuzitafakari na kuzifanyia kazi ili uchumi uweze kwenda kwa kasi zaidi tuwaondoe wananchi wetu kwenye umasikini na vijana wetu wapate kazi’ Alisema Dkt. Mpango.

Alisema wakati wa kuandaa bajeti yam waka 2018/2019, serikali itaweka mfumo wa kodi utaoiwezesha Sekta Binafsi kukua na kuimarika zaidi ili iweze kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi na kuboresha maisha ya watanzania kwa ujumla.

“Katika mjadala huu nimefurahia kusikia maoni ya sekta binafsi ambapo pamoja na kupendekeza maeneo ya kupunguza kodi, lakini pia wamezungumzia namna ya kuongeza wigo wa kuongeza mapato ya Serikali” Aliongeza Dkt. Mpango.

Hata hivyo, Dkt. Mpango, alitahadharisha jumuiya ya wawekezaji na wafanyabiashara nchini kwamba wanapojadili juu ya masuala ya kodi, wakumbuke kwamba Serikali ina mzigo mkubwa wa kuhudumia jamii katika masuala mbalimbali ikiwemo elimu, maji, afya, barabara, miundombinu ya usafiri na usafirishaji ikiwemo reli na mingine mingi.
Alitolea mfano uzalishaji wa maji katika miji mikuu ya Wilaya na miji midogo ni lita milioni 99.5 kwa siku wakati mahitaji ni lita milioni 273 kwa siku, sawa na 36.4%.

“Miradi ya maji ya Kitaifa uzalishaji ni lita milioni 59.5 ikilinganishwa na mahitaji ya lita 119 kwa siku, sawa na 50% ya mahitaji” Alisisitiza Dkt. Mpango

Alibainisha kuwa vifo vitokanavyo na uzazi ni 556 katika kila vizazi hai 100,000 wakati lengo ni kuvipunguza visizidi vifo 265 katika kila vizazi hai 100,000 itakapofika mwaka 2020.

Aidha Dkt. Mpango alisema kuwa huduma za msingi zinazotolewa na Serikali hususan, ulinzi wa nchi, usalama wa raia, na mali zao, utawala, usimamizi wa rasimali za nchi, na ujenzi wa miundombinu ya msingi isiyo na mvuto kwa sekta binafsi, lazima ziendelee kugharamiwa na Serikali.

Dkt. Mpango alielezea pia namna misaada na mikopo kutoka kwa wadau wa maendeleo inavyopungua mwaka hadi mwaka ambapo alisema mikopo yenye masharti nafuu ilishuka kutoka shilingi trilioni 1.3 mwaka 2013/14 hadi shilingi bilioni 495 mwaka 2015/2016

Alifafanua kuwa misaada kutoka kwa washirika hao wa maendeleo imeshuka kutoka shilingi trilioni 1.5 kwa mwaka 2013/2014 hadi sh. Trilioni 1.23 mwaka 2015/2016.

Vilevile alieleza kuwa kiwango cha ulipaji kodi kwa hiari miongoni mwa wafanyabiashara na wawekezaji bado hakiridhishi na ukwepaji kodi/uvujaji wa mapato ya Serikali bado ni matatizo sugu hivyo kuitaka Sekta Binafsi iyatupie macho mambo hayo wakati wakijadili na kushauri namna Serikali inavyoweza kuboresha kodi ili mambo hayo ya msingi ya kuihudumia jamii yasikwame

Wakizungumza kwa niaba ya Sekta Binafsi, Mwenyekiti wa Shirikisho la wenye viwanda hapa nchini Dokta Samuel Nyantahe na mmoja wa wafanyabiashara Bw. Boaz Ogola, wameishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa nia yake ya dhati ya kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara hapa nchini na kwamba wako tayari kushirikiana nayo ili kutimiza azma yake ya kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 kwa kuwa wameiona nia njema ya Serikali ya kufikia hatua hiyo

Mkutano huo wa siku moja umewakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi huku agenda kuu ya mkutano huo ilikuwa kujadili kwa undani masuala mbalimbali ya kodi ambapo Sekta binafsi imependekeza mambo kadhaa ambayo Serikali imeahidi kuyafanyiakazi.

No comments:

Post a Comment

Pages