WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amewatoa hofu wakazi 1,000 wa Manispaa ya Songea wanaoidai
fidia ya sh. bilioni 3.8 ya eneo lao ambalo limechukuliwa na kuwa eneo la
kiuchumi mkoani Ruvuma (Ruvuma SEZ) kwa ajili ya ujenzi wa viwanda.
Ametoa
ahadi hiyo leo (Jumamosi, Desemba 23, 2017) wakati akizungumza na wakazi wa
kata ya Mwengemshindo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Manispaa
hiyo.
Amesema
Serikali ya awamu ya tano inatambua kilio chao ambacho alisema ni cha muda
mrefu na kwamba alishawahi kupata ombi maalum kutoka kwa mbunge wao wa zamani,
Bw. Leonidas Gama ambaye sasa ni marehemu.
“Alipotoka
kutibiwa India alikuja ofisini kwangu na kunieleza kwamba ana mambo mawili ambayo
nikifanya ziara mkoani Ruvuma anaomba niyatafutie ufumbuzi. La kwanza lililkuwa
ni hili la fidia kwa wakazi wa Mwengemshindo na la pili lilikuwa ni la ujenzi
wa kituo cha mabasi cha mjini Songea,” alisema.
“Leo
nimefanya ziara maalum kwa ajili yenu kwa sababu serikali ya awamu ya tano iko kwa
ajili yenu na hasa wananchi wanyonge. Na tatizo hili inalijua. Kabla sijafika
hapa, nilipita kwenye eneo husika na afisa mipango miji akanionyesha ramani ya
eneo lenu hili,” alisema.
Waziri Mkuu
aliwaeleza wakazi hao kwamba eneo hilo limetengwa na Manispaa kwa ajili ya
ujenzi wa viwanda ambapo wawekezaji watatu tayari wamekwishajitokeza na wanataka
kujenga viwanda vitatu.
“Kutakuwa na
kiwanda cha kusindika mahindi, kutengeneza pumba za kuku na ng’ombe na mbolea.
Kiwanda cha pili kitakuwa ni cha kusindika kahawa na cha tatu kitakuwa ni cha
kukamua mafuta ya mbegumbegu,” alisema na kuongeza kwamba reli ya kutoka Mtwara
kwenda Mbaba Bay inatarajiwa kupita kwenye eneo hilo.
Akitoa
ufafanuzi kuhusu kuchelewa kwa amlipo yao, Waziri Mkuu alisema kwamba katia ya
wawekezaji hao watatu aliyekwishalipa fidia ni mmoja tu, na kwamba kwa mujibu
wa sheria ya uwekezaji, fidia inapaswa kulipwa na mnunuzi wa eneo husika.
Hata hivyo,
Waziri Mkuu alikiri kuwepo kwa mapungufu wakati wa ulipaji kwa sababu walifuata
orodha ya majina (kialfabeti) badala ya kutoa malipo kwa wakazi wa eneo husika.
“Sasa hivi mwekezaji anataka kuanza ujenzi, lakini ndani ya eneo lake kuna watu
ambao bado hawajalipwa, kwa hiyo hawawezi kutoka hadi wale waliobakia nao
walipwe. Serikali itawafuatilia hawa wawekezaji wengine ili nao walipe fedha
zao haraka ili waliobakia waweze kulipwa,” alisema.
Jumla ya
watu 2,179 walifanyiwa uthamini mwaka 2008 na gharama yao kubainika kuwa ni sh.
3,254,737,622. Kuanzia Juni 8-19, 2015, Serikali iliwalipa wakazi 1,179 sh. 1,920,242,121
ambapo kati ya hizo, sh. 1,210,078,261 zilikuwa ni malipo ya thamani ya mali za
wananchi na sh. 710,163,860 zilikuwa ni riba kutokana na malipo hayo kuchelewa
kufanyika.
Eneo hilo
lenye ukubwa wa hekta 2,033 (sawa na ekari 5,000) lilitwaliwa na Mamlaka ya
Ukanda Maalum wa Uwekezaji (EPZA) kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa wa Ruvuma
na Manispaa ya Songea tangu mwaka 2007. Eneo hilo linajumuisha mitaa ya
Luwawasi (Mkuzo), Mwengemshindo na Luhira.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu
amemuagiza Afisa Ardhi wa Manispaa ya Songea, Bw. Ndemfoo Kundaeli Fanuel afuatilie
suala la Bibi Monica Joseph Miti na wanae ambao walidhulumiwa nyumba ya urithi na
aliyekuwa mwanasheria wa manispaa hiyo.
Ametoa
agizo hilo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kata ya Mwengemshindo
baada ya kupokea bango lililoandikwa na Bibi Miti kuomba arejeshewe umiliki wa
nyumba ya marehemu muwewe.
Alipopewa
nafasi ya kueleza tatizo lake, Bibi Miti ambaye alimtaja mwanasheria huyo kwa
jina moja la Bw. Mwakasungura, alidai kuwa mwanasheria huyo alighushi hati ya
nyumba, na kuwatoa ndani ya nyumba yeye na watoto wa marehemu.
Alipoulizwa
na Waziri Mkuu aeleze alipo huyo mwanasheria wa manispaa, Mkurugenzi wa
Manispaa hiyo, Bibi Tina Sekambo alijibu kwamba alishahamishiwa wilaya ya
Ukerewe.
Waziri Mkuu
amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea na Afisa Ardhi wa Manispaa wafuatilie
suala hilo na wampe majibu mapema iwezekanavyo. Pia amemuomba Bibi Miti na
wanawe wafike kuonana naye Januari 3, mwakani atakapokuwa Songea kwa mapumziko
mafupi ya mwisho wa mwaka.
Waziri Mkuu
amemaliza ziara yake ya siku moja mkoani Ruvuma.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, DESEMBA 23, 2017.
No comments:
Post a Comment