WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko ya Zanzibar kuhakikisha inatumia Tamashara la Biashara la Zanzibar kama chachu ya kukuza biashara ya Utalii kama ilivyo kwa Dubai Shooping Festival na matamasha mengine Duniani.
“Natambua kwamba kazi ya
kulipandisha hadhi zaidi tamasha letu hili si ndogo , hata hivyo ninayo imani
kubwa kwamba si tu uwezo wa kufikia
malengo hayo mnayo bali pia mnaweza.”
Waziri Mkuu aliyasema hayo
jana jioni (Jumatano, Januari 10, 2018) wakati akifungua Tamasha la Nne la
Biashara la Zanzibar lililofanyika kwenye viwanja vya Maisara katika mkoa wa
Mjini Magharib, wilaya ya Mjini.
Tamasha hilo lilifunguliwa jana
ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za kuelekea katika sherehe za kuadhimisha
miaka 54 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, ambayo yalitokea Januari 12, 1964.
Alisema Wizara ya Biashara,
Viwanda na Masoko inatakiwa kutumia fursa ya uwepo wa tamasha hilo katika
kuhakikisha inakuza biashara ya Utalii kwa kuwa linajumuisha wafanyabiashara
kutoka mataifa mbalimbali.
Waziri Mkuu alisema Tamasha
la Biashara ni nyenzo muhimu ya kukuza biashara na huduma pamoja na kukuza
uchumi wa nchi, pia linatoa fursa ya kuwakutanisha wafanyabiashara au watoa
huduma na wateja wao.
”Hali hii humuwezesha
mzalishaji kupata mrejesho kuhusu namna bidhaa yake inavyokubalika kwenye soko,
mapungufu yaliyopo kwenye bidha husika pamoja na kuelewa maboresho anayotakiwa
kuyafanya katika bidhaa au huduma.”
Waziri Mkuu alisema kuwa
tamasha hilo linaweza kutumika kama nyenzo muhimu katika kuanzisha mahusiano
mazuri ya kibiashara kati ya mteja na
mfanyabiashara, hivyo kuwawezesha wajasiriamali kuwa na masoko ya uhakika.
Pia Waziri Mkuu alisema
kufanyika kwa tamasha hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM) ya mwaka 2015 katika ibara ya 84 (f).
“Ilani imeweka wazi azma ya
Serikali ya kuanzisha na kuendeleza ujenzi wa kiwanja cha maonyesho ya biashara
cha kimataifa na kuhakiisha ushiriki wa wajasiriamali wa Zanzibar katika maonyesho ya biashara ya kimataifa
ndani na nje ya nchi.”
Baada ya kufungua tamasha
hilo Waziri Mkuu alitembelea mabanda mbalimbali katika viwanja yakiwemo ya
taasisi za umma pamoja na wajasiriamali ambao wanatoka Zanzibar, Tanzania Bara,
Kenya, Uturuki, Misri, Uganda na Burundi.
Awali, Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko
Zanzibar Balozi Amina Salum Ali alisema tamasha hilo lenye washiriki zaidi ya
200 limeandaliwa na wizara yake pamoja na TanTrade.
Balozi Amina aliseka kauli
mbiu ya tamasha hilo kwa mwaka 2018 ni ‘wekeza kwenye viwanda kwa uchumi na
ajira’ inalengo la kuhamasisha wadau kuongeza uelewa kwa wananchi juu ya
falsafa na dhima ya ujenzi wa viwanda.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
ALHAMISI, JANUARI 11, 2018.
No comments:
Post a Comment