WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itawachukulia hatua
watendaji wote watakaobainika kuhujumu ujenzi wa miradi ya maji mkoani Mara.
Hatua hiyo imetokana na kutoridhishwa na utekelezwaji wa ujenzi miradi
ya maji katika baadhi ya halmashauri za mkoa huo,hivyo kuwacheleweshea wananchi
kupata huduma hiyo.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Januari 16, 2018)
wakati alipokagua mradi wa maji wa Utegi uliopo katika kijiji cha Mika wilayani
Rorya.
Amesema Serikali inatekeleza Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo. Kampeni
hiyo inalenga kuwaondolea wananchi
tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.
Waziri Mkuu
amesema malengo ya kampeni hiyo ni kuwafikishia wananchi huduma ya maji safi na
salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.
“Nitafuatilia
katika maeneo yote ili kujua kama kiasi cha fedha kilichotolewa kwa ajili ya
kugharamia miradi mbalimbali ya maji kinalingana na thamani halisi ya miradi
husika.”
Waziri Mkuu
amesema anakerwa na Halmashauri ya wilaya ya Rorya kutosimamia vizuri miradi ya
maji inayotekelezwa katika wilaya hiyo, ikiwa ni pamoja na kutozingatia sheria.
Wakati huo huo Waziri Mkuu amewataka watumishi wote wa Halmashauri ya wilaya ya
Rorya wanaoshi wilayani Tarime wawe wamehamie Rorya ifikapo Februari 15, 2018.
“Atakayeng’ang’ania
kuishi Tarime hadi siku hiyo atakuwa amejiondoa kazini mwenyewe. Lazima
watumishi wote waishi kwenye vituo vyao vya kazi Rorya ili waweze kutekeleza
majukumu yao ipasavyo.”
Pia Waziri Mkuu
aliwataka wananchi wa wilaya hiyo kutojihusisha na vitendo vya kihalifu ikiwemo
ulimaji wa bangi pamoja na uvuvi haramu na badala yake wafanye shughuli halali
za kuwaingizia vipato.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMANNE, JANUARI 16, 2017.
No comments:
Post a Comment