*Amuagiza CAG kufanya uchunguzi tangu
kuanzishwa kwake
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameuvunja Mfuko wa Wakfu wa
Kuendeleza zao la Kahawa (CDTF) na amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) kuchunguza
mwenendo wa mfuko huo tangu ulipoanzishwa.
Ametoa agizo hilo leo (Jumapili, Januari 14, 2018) wakati akizungumza
na wadau wa zao hilo kwenye kikao cha kujadili maendeleo ya zao la kahawa alichokiitisha,
mjini Dodoma.
Waziri Mkuu amechukua hatua hiyo baada ya kubaini kwamba uundwaji
wa mfuko huo si wa kisheria bali ni wadau wa zao hilo kwa kushirikiana na Bodi
ya Kahawa Tanzania (TCB).
“Wakati Serikali inapambana kupunguza makato ya hovyo kwa
wakulima, kumbe huku kuna chombo cha kuwachukulia fedha wakulima hii
haikubaliki.”
Pia aliagiza kufungwa kwa ofisi za CDTF ili kupisha uchunguzi na
baada ya CAG kukamilisha uchunguzi na kukabidhi ripoti, kazi zote zilizokuwa
zinafanywa na mfuko huo zitafanywa na Bodi ya Kahawa.
Hata hivyo, Waziri Mkuu ameongeza kuwa majukumu ya kuundwa kwa mfuko huo yanaingiliana
na yale ya Bodi ya Kahawa, ambayo ni pamoja na kufuatilia maendeleo ya zao
hilo, hivyo hakuna haja ya kuwa vyombo viwili vinavyofanya kazi moja.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amepiga marufuku wanunuzi
wa kahawa kwenda kununua kwa wanavijiji na badala yake kahawa yote itauzwa kwa
njia ya minada.
“Kahawa itauzwa katika minada tu na utaratibu wa kutoa vibali
kwa wanunuzi wa kahawa kwenda kununua kwa wananchi vijijini marufuku kuanzia
sasa, kama kuna watu wamepeleka fedha zao wazirudishe kwani hazitafanya kazi.”
Amesema Wakuu wa Mikoa na Wilaya wasimamie uuzwaji wa zao hilo
na kuwachukulia hatua wote watakaokutwa wananunua kahawa kwa wakulima.
“Anayetaka kahawa akanunue mnadani na si kwa wanavijiji lengo ni kuhakikisha
mkulima anapata tija.”
Pia ameziagiza halmashauri zote zinazolima kahawa nchini
kuanzisha vitalu vya miche ya kahawa na kisha kuigawa bure kwa wakulima, pia Maofiza
Kilimo wawaelimishe walkulima wote wenye miti mikongwe waanzisha mashamba mapya.
Kuhusu suala la utafiti wa zao hilo, Waziri Mkuu ameiagiza
Wizara ya Kilimo itumie vyuo vyake vya kilimo ianzishe vituo vyake vya utafiti
vitakavyofanya kazi ya utafiti wa zao hilo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Bw. Joseph Kakunda amesema watahakikisha
maagizo hayo yanafanyiwa kazi, ambapo aliwaagiza Wakuu wa mikoa yote 16
inayolima kahawa pamoja na wakuu wa wilaya wake 52 wahakikishe wanafuta mara
moja vibali vya ununuzi wa kahawa katika vyanzo vyao vya mapato.
Kikao
hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Hazina mjini Dodoma kilihudhuliwa na
Waziri wa Kilimo Dkt. Chales Tizeba, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji
Bw. Charles Mwijage, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Bw. Kakunda.
Wengine
ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu,, Bibi Maimuna Tarishi, Katibu Mkuu Wizara
ya Kilimo, Mhandisi Mathew Mtigumwe, Wakuu wa mikoa 16 wanaolima kahawa na wakuu
wa wilaya,Mrajis wa Vyama vya Ushirika Nchini, Dkt. Tito Haule, Makatibu tawala
wa mikoa inayolima kahawa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa na wajumbe wa bodi hiyo,,Mkurugenzi wa bodi
ya Kahawa Tanzania, Wakurugenzi wa Halmashauri,
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAPILI, JANUARI 14, 2017.
S. L. P. 980,
DODOMMA
No comments:
Post a Comment