WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemkabidhi Mhandisi wa Maji wa
Halmashauri ya wilaya ya Rorya, Mhandisi Obetto Sasi kwa Naibu Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Bw. Josephat Kandege baada ya kutoridhishwa na utendaji
wake.
Ametoa uamuzi huo jana jioni (Jumanne, Januari 16, 2018) wakati
aliposimamishwa na umati wa wananchi kwenye mji Mdogo wa Shitari alipokuwa
njiani kuelekea kwenye kijiji cha Bubombi wilayani Rorya.
“Hatuwezi kuwa na mtumishi wa aina hii ambaye kila eneo
tunakutana na changamoto za maji huku kukiwa hakuna hatua zinazochukuliwa licha
ya Serikali kutoa fedha, hivyo namuagiza Katibu Tawala wa Mkoa alete mhandisi
mwingine wa maji.”
Pia Waziri Mkuu amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na
Umwagiliaji Profesa Kitila Mkumbo kwenda wilayani Rorya na kukagua mradi wa
maji katika mji Mdogo wa Shirati na kuona namna ya kuutekeleza.
Amesema kwa sasa Serikali inatekeleza Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama
ndoo. Kampeni hiyo inalenga kuwaondolea
wananchi tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, hivyo
itawachukulia hatua wote watakaokwamisha miradi ya maji.
Awali, Mkuu wa
Mkoa wa Mara Bw. Adam Maliwa alimueleza Waziri Mkuu kwamba changamoto ya
upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika mkoa huo inatokana na
watendaji wa idara hiyo kutokuwa na uwezo wa kutosha kiutendaji.
Wilaya ya Rorya
inatekeleza miradi 11 ya maji ya bomba kupitia Programu ya Maji na Usafi wa
Mazingira Vijijini (RWSSP) katika vijiji vya Kinesi, Randa, Utegi, Mika,Kirogo,
Nyihara, Kisumwa,Nyamkonge, Nyambori, Gabimori na Marasibora.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMATANO, JANUARI 17, 2017.
No comments:
Post a Comment