HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 25, 2018

KAMATI YA MALIASILI YATOA MILIONI 80 KUSAIDIA KIJIJI ULANGA-KILOSA

NA MWANDISHI WETU

KAMATI ya Maliasili ya Kijiji cha Ulaya Mbuyuni wilayani Kilosa mkoani Morogoro imetoa zaidi ya shilingi milioni 80 kwa ajili ya maendeleo ya kijiji kwa kipindi cha mwaka 2014 hadi 2018.

Hayo yamesemwa na Katibu wa Kamati hiyo Victoria Ndekelo wakati akiwasilisha ripoti ya Kijiji kuhusu Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS ) mbele ya Mkuu wa Wilaya hiyo Adam Mgoi ambaye alitembelea kijiji hicho kuangalia mradi unavyotekelezwa.

Mradi huo wa TTCS unatekelezwa na Shirika la Kuhifadhi Misitu Asili Tanzania (TFCG), Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (Mjumita) na Shirika la Kuendeleza Nishati Tanzania (TaTEDO) kwa  ufadhili Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Uswiss  (SDC).

Alisema kamati hiyo imefanikiwa kupata zaidi ya shilingi milioni 100 katika miradi mbalimbali kama kukata mkaa, kuuza asali, mbao, kilimo na vikoba hali ambayo imewasukuma kutoa zaidi sh.milioni 80 kwa ajili ya maendeleo ya kijiji.

"Kipindi cha mwaka 2014 hadi 2018 kamati ya kijiji ya maliasili imetoa shilingi milioni 15.5 kwa ajili ya ujenzi wa darasa milioni 20.1 kuchimba kisima, milioni 2.6, ujenzi wa ofisi ya kijiji, milioni 4.7 ujenzi wa maabara, milioni 20 kwa utunzaji wa misitu, milioni 10 ujenzi wa darasa moja na milioni 10.3 itatumika kwa ajili ya usimamizi wa misitu, " alisema.

Alisems katika mradi wa ukataji mkaa endelevu wanakijiji 83 ambapo wanaume 68 wanawake 15 ambao wanajiingizia kipato na kuhudumia familia zao katika kutatua changamoto za maisha.

Ndekelo alisema wanakijiki hao wanakata mkaa katika eneo la hekta 250 ambapo mkaa utavunwa katika vitalu 37 kwa mwaka kati ya eneo lote la hekta 3,540 huku eneo lilibakia likijihusisha na uvunaji mbao, kuni na hifadhi ya maji na bionowayi.

Alisema matarajio yao ni kufanya uvunaji wa msitu huo kwa miaka 24 huku wakihakikisha kuwa msitiu unauwa endelevu kwa vizazi vijavyo.

Katibu huyo alisema kijiji kina viundi vinne vya kuweka na kukopa vyenye wanachama 114 wanawake 61 wanaume 53 ambao hadi wana mtaji wa shilingi milioni 34.6.

“Kilimo hifadhi wapo wakulima 72 wanawake 38 wanaume 34, mradi wa nyuki wanachama 20, pia kijiji kina mpango wa matumizi bora ya ardhi kama mpango wa usimamizi shirikishi wa misitu ili iwe endelevu,” alisema.

Katibu huyo alisema pamoja na jitihada ambazo zinafanyika kutunza misutu na mazingira sera iliyopo haitoi nguvu kwa vikundi husika hivyo kuiomba Serikali kufanyia marekebisho sera husika.

Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo Mkuu wa wilaya Mgoi alitoa maagizo kwa halmashauri ya Kilosa kuhakikisha kuwa mradi huo unafikia vijiji vyote 139 vilivyopo wilayani hapo ili kuunga mkono jitighada za wahisani.

Mgoi alisema iwapo hakutakuwa na msukumo wa Serikali kusambaza ujumbe huo wa utunzaji mazingira na misitu huku shughuli za ukataji mkaa endelevu ni dhahiri Kilosa itakuwa jangwa.
“Kilosa tumebarikiwa kuwa na misitu lakini kama hakutakuwa na jitihada za kushirikiana na wadau katika kuitunza ni wazi haitadumu kwani vijiji 20 ambavyo vimefikiwa ni vichache ukilinganisha na idadi ya vijiji 139 tulivyonavyo,” alisema.
Mgoi alisema halmashauri inapaswa kutenga bajeti ya kutekeleza miradi ya uhifadhi mazingira na misitu kuanzia mwaka wa fedha wa 2018/19 ili utekelezaji wa  mradi huo uanze mara moja.
Alisema halmashauri inapaswa kutumia wanakijiji walioshiriki katika miradi iliyopo vijiji 20 vya awali ili kuweza kurahisisha kazi hiyo kwa wakati mfupi.
“Mradi huu umekuwa na matokeo chanya katika maebneo mawili moja wananchi wamenufaika kwa kupata kipato, pili miradi ya Serikali imetekelezwa kwa asilimia 100 kupitia fedha za mradi hii ndio miradi inahitajika na mimi nitawaunga mkono ila kuweni makini na wapenda maslahi binafsi,” alisema.
Mkuu huyo wa wilaya aliwataka watendaji kuanzia ngazi ya chini kusimamia majukumu yao na sheria ili kuhakikisha migogoro mbalimbali inayotokea inatatuliwa kwa wakati na sio kwenda kwa mkuu wa wilaya.
Alisema iwapo wenyeviti au watendaji mbalimbali watashindwa kuchukua au kutatua migogoro katika maeneo yao hatua zitachukuliwa bila uoga.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kilosa Hassan Mkopi alisema watahakikisha kuwa bajeti ya mwaka huu inakuwa na fungu linalohusu utekelezaji wa miradi ya utunzaji wa mazinmgira na maliasili.
Kwa uoande wake Mshauri wa Maliasili wa Mkoa wa Morogoro, Joseph Chuwa alisema matunda ambayo yamepatikana Kilosa katika vijiji 20 yanapaswa kufikia wilaya zote za mkoa huo pamoja na nchi kwani yana tija.

No comments:

Post a Comment

Pages