WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka
mabalozi watumieni mbinu za kidiplomasia kuvutia wawekezaji katika sekta mbalimbali
ikiwemo ya utalii na kutafuta masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini.
Pia Waziri Mkuu amewataka mabalozi hayo wakaimarishe
diplomasia kwa lengo la kuzifanya nchi hizo ziendelee kushirikiana na Tanzania katika
shughuli za kiuchumi na kijamii.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi,
Febriari 24, 2018) wakati akizungumza na Balozi Dkt. Wilbrod Slaa
anayewakilisha Tanzania nchini Sweden na Balozi Muhidin Ally Mboweto anayewakilisha Tazania
nchini Nigeria, katika
makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu amesema Tanzania ina
vivutio vingi vya utalii kama uwepo wa fukwe za bahari kuanzia Tanga hadi
Mtwara, maziwa na mito, mbuga za wanyama hivyo ni vema wakajielekeza katika
kuvutia wawawekezaji kwenye sekta hiyo ili Taifa lipate watalii wengi.
Amesema mbali na kutangaza sekta ya
utalii, pia watafute wawekezaji kwa ajili ya kuwekeza kwenye sekta ya madini,
viwanda na kutafuta masoko ili wafanyabiashara na wakulima wa Tanzania waweze
kuuza bidhaa zao nje ya nchi.
“Tumejiimarisha katika mazao ya
chakula na biashara, hivyo tunatakiwa kuwa na uhakika wa masoko kwenye kilimo ili
mkulima anapozalisha pamba, tumbaku, kahawa, chai, korosho, dengu pamoja na
mazao mengine tuwe na mahali pa kuuza, kwa hiyo washawishini wafanyabiashara
kuja kununua.”
Pia Waziri Mkuu amewataka mabalozi hao wakawatambue na kuwaunganisha
Watanzania waishio kwenye nchi wanazoiwakilisha ili nao washiriki kwenye ujenzi
wa uchumi wa viwanda na wawasisitize wafuate sheria za nchi wanazoishi na
wakumbuke nyumbani.
Waziri Mkuu amewasisitiza mabalozi hao kwenda kupunguza gharama
za uendeshaji wa Balozi kwa kuzuia matumizi katika mambo yasiyo ya lazima. “Pia
maslahi ya nchi lazima mkayasimamie huko muendako hasa katika masuala ya kiuchumi”
Kwa upande wao mabalozi hao wamesema watahakikisha
wanayafanyia kazi maelekezo yote waliyopewa ikiwa ni pamoja na kuimarisha
ushirikiano baina ya Tanzania na nchi wanazoziwakilisha.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, FEBRUARI 24,
2018.
No comments:
Post a Comment