NA MWANDISHI WETU
KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday, ameteuliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Fedha kwa nchi za ukanda wa tano (EAAR).
EAAR inaundwa na vyama na mashirikisho ya Riadha ya nchi 11, ambazo ni Kenya, Uganda, Ethiopia, Sudan, Sudan Kusini, Eritrea, Djibouti, Burundi, Somalia, Zanzibar na Tanzania Bara.
Uteuzi huo ulifanyika baada ya mkutano mkuu wa EAAR uliofanyika mwishoni mwa mwezi uliopita nchini Kenya na taarifa kufika RT wiki hii.
Gidabuday katika kamati hiyo anaungana na Bililign Makoya (Ethiopia), Peter Angwenyi (Kenya), na Saddiq Ibrahim (Sudan), ambaye pia ni Katibu Mkuu wa EAAR.
Akizungumzia uteuzi huo, Gidabuday alisema ni fahari kwa Tanzania na kwamba atatekeleza majukumu yake ipasavyo.
“Kazi kubwa ya kamati hii ni kusaka fedha kwa ajili ya kuandaa mashindano mbalimbali na mwaka huu mashindano ya vijana yanatarajiwa kufanyika nchini Tanzania mwezi Mei,” alifafanua zaidi Gidabuday.
Gidabuday, anatarajiwa kuhudhuria mkutano mkuu wa EAAR utakaofanyika Machi 23 nchi Hispania kabla mashindano ya Dunia ya Nusu Marathon.
No comments:
Post a Comment