CHANGAMOTO ya upatikanaji
wa huduma za afya iliyokuwa inawakabili wakazi wa kijiji cha Mbecha kata ya
Nanganga imekuwa historia baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuweka
jiwe la msingi la ujenzi wa zahanati.
Amesema wakazi hao walikuwa
wakipata shida ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya katika vijiji
vya jirani mara mtu anapougua ikiwa ni pamoja na dharura mbalimbali zikiwemo za
wajawazito.
Waziri Mkuu ambaye ni mbunge
wa jimbo la Ruangwa ameweka jiwe hilo la msingi leo (Alhamisi, Machi 01, 2018),
alipowasili mkoani Lindi kwa ziara ya kikazi katika jimbo la Ruangwa. Ujenzi wa
zahanati hiyo umefadhiliwa na African Relief Organisation.
“Mbecha mtu akiugua tulikuwa
tunapata shida ya sehemu ya kupata huduma za matibabu, leo matibabu yatakuwa
yanapatikana hapa kijijini. Kwa niaba ya Wanaruangwa nawashukuru sana viongozi
wa African Relief Organisation”.
Waziri Mkuu amesema kuwa
mkakati wa Rais Dkt. John Magufuli ni kuimarisha sekta ya afya kwa kujenga na kuboresha vituo vya
afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya karibu na makazi yao.
Awali, Mtendaji wa Kijiji cha Mbecha, Bw.
Alfan Ngaeje alisema wazo la ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho lilianza 1987,
ambapo utekelezaji wake ulikwama kutokana na hali duni ya kiuchumi iliyokuwa
ikiwakabili wakazi wake.
Alisema wananchi wengi
waliendelea kupata shida ya kupata huduma za afya hasa akinamama wajawazito na
watoto waliokuwa wakitembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo kwenye zahanati za
vijiji vya jirani.
Hivyo alimshukuru Waziri Mkuu
kwa niaba ya wakazi wa kijiji hicho kwa kuwatafutia mfadhili aliyewajengea
zahanati hiyo ambayo ipo katika hatua za mwisho kukamilika.
Mtendaji huyo alisema huduma
zitakazokuwa zinatolewa kwenye zahanati hiyo ni pamoja na matibabu ya wagonjwa wa
nje (OPD), kliniki kwa wajawazito na watoto, chanjo na uzazi wa mpango.
Huduma nyingine ni kuzuia
maambukizi wa virusi vya ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, kujifungua,
elimu ya kujikinga na mangonjwa mbalimbali. Jumla ya kaya 594 zenye wakazi
2,485 wanatarajiwa kunufaika na zahanati hiyo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, MACHI 01,
2018.
No comments:
Post a Comment