HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 06, 2018

SMZ: TUENZI KUMBUKUMBU YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR

Na Talib Ussi
 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na mamlaka husika itatafakari namna bora zaidi ya kukusanywa kwa Kumbukumbu muhimu za Kiongozi wa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Aman Karume ili ziwe kielelezo cha Taaluma kwa Kizazi cha sasa.


Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo baada ya kuyapokea Matembezi Maalum ya Vijana 400 wa Chama cha Mapinduzi ya kumuenzi Mzee Abeid Aman Karume yaliyoanzia Kijiji alichozaliwa cha Mwera Kiongoni na kumalizia katika Viwanja vya Afisi Kuu ya CCM Kisiwanduzi Mjini Zanzibar.


Alisema Kumbukumbu hizo ndio njia pekee ya kuendelea kumuenzi Kiongozi huyo kwa kufuata fikra na mawazo aliyowaachia Wananchi wa Zanzibar wakielewa kwamba yeye ndie aliyeongoza mapambano dhidi ya Wakoloni na hatimae kupatikana kwa Ukombozi wa Visiwa vya Zanzibar.


“Lazima tuenzi yale aliyotuachia kiongozi wetu, na itakuwa elimu tosha kwa vijana wetu wa leo” alieleza


Balozi Seif aliwataka Vijana kutambua wajibu wao kwa kuepuka sambamba na hilo Balozi Seif aliwataka vijana hao kudumisha umoja wao ili wazidi kuendeleza fikra zao hizo kwa viongozi wao ambao waliikomboa Zanzibar.


Alisema Serikali zote mbili nchini Tanzania pamoja na Chama cha Mapinduzi ziko madhubuti katika kuwatumikia Wananchi wake huku zikielewa kuwategemea Vijana wake wanaopaswa kulitambua hilo bila ya kukata tamaa pale zinapotokea changamoto mbali mbali.


Balozi Seif aliwatahadharisha Vijana kutambua kwamba bado wapo Watu wanaodhani kwamba Sultani na Vibaraka wao waliopeperushwa katika Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari Mwaka 1964 wanaendelea na kasumba ya kuhisi wameonewa.


Alitanabahisha na kuweka wazi kwamba Mapinduzi hayo ya Januari Mwaka 1964 ndio yaliyoleta Heshima na Utu wa Mwafrika wa Zanzibar na Watanzania wote ikiwa ni chanzo kikubwa cha Umoja wa Wananchi wote wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.


Mapema akitoa Taarifa ya Matembezi hao Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM { UVCCM} Zanzibar Nd. Abdulghafar Idrisa aliushukuru Umoja wa Askari Wastaafu Zanzibar (UMAWA) kwa msimamo wao wa kuwaunga mkono Vijana katika Matembezi hayo.
 
Abdulghafar alisema Uzalendo wa Wazee hao umeonyesha jinsi gani walivyojikubalisha kuendelea kuyaunga Mapinduzi ya Zanzibar yaliyoongozwa na Jemadari wao Marehemu Mzee Karume aliyeuawa kikatili na wapinga Maendeleo wa Visiwa vya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

Pages