*Lengo ni kuhamasisha
wanaume wapime afya zao, wajue hali zao
*Ataka Wakuu wa Mikoa
wahamasishe upimaji hadi ngazi za vijiji
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema mwezi ujao, atazindua kampeni maalum ya upimaji wa virusi vya UKIMWI
(VVU) ambayo imelenga kuwahamasisha wanaume wapime afya zao na kutambua hali
zao.
“Serikali tumeandaa kampeni
maalum ya kuhamasisha upimaji wa VVU na kuanza matumizi ya dawa za kufubaza VVU
mara moja (Test and Treat), hasa kwa wanaume. Kampeni hii itazinduliwa rasmi na
mimi mwenyewe jijini Dodoma tarehe 19 Juni 2018,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Mei 30, 2018)
wakati akizindua maadhimisho ya miaka 15 tangu
kuanzishwa kwa Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Kudhibiti
Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI
(PEPFAR) kwenye ukumbi wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam.
“Takwimu zinaonyesha watu ambao wako
tayari kupima kwa hiyari yao siku zote ni wanawake. Akinababa wakiambiwa hutoa
sababu mara hiki, mara kile. Nitoe wito kwa wanaume wote, tubadilike! Ni vema
tushiriki kampeni ya wanaume kujitambua na kupima ili tujue hali zetu,” amesema.
Amewataka wadau wote
wanaohusika na masuala ya UKIMWI washiriki kikamilifu katika kampeni hiyo baada
ya uzinduzi, na pia akawataka Wakuu wa Mikoa mikoa yote nchini wasimamie kampeni hizo
muhimu katika mikoa yao
hadi ngazi ya vijiji.
Waziri Mkuu amesema ujio wa PEPFAR
umeleta mafanikio makubwa katika vita dhidi ya UKIMWI na kupitia shughuli zake,
elimu ya kinga na ufahamu kuhusu UKIMWI ilitolewa kwa watu wa rika na makundi
mbalimbali ya jamii.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Tanzania
bado inakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo ukubwa wa viwango vya maambukizi
na kuongezeka kwa idadi ya watu wanaoambukizwa VVU katika baadhi ya mikoa
nchini.
Amesema kuna mikoa 14 ambayo kiwango
cha maambukizi kiko juu ya wastani wa kitaifa wa asilimia 4.7 na akaitaja mikoa
hiyo kuwa ni Njombe wenye asilimia 11.4, Iringa (asilimia 11.3), Mbeya (asilimia
9.3), Mwanza (asilimia 7.2), Kagera (asilimia 6.5) na Katavi (asilimia 5.9).
Mikoa mingine ni Shinyanga (asilimia 5.9), Songwe (asilimia 5.8) Ruvuma (asilimia
5.6) Pwani (asilimia 5.5) Tabora (asilimia 5.1) pamoja na Tanga, Dodoma na
Geita ambayo yote ina asilimia 5.0 ya maambukizi.
Waziri Mkuu ameitaja mikoa
mingine sita ambayo ina ongezeko kubwa la watu wanaoishi na VVU kuwa ni Iringa
(asilimia 11.3), Mwanza (asilimia 7.2), Kagera (asilimia 6.5), Tanga (asilimia 5.0),
Dodoma (asilimia 5.0) na Manyara (asilimia 2.3).
Amesema takwimu hizo
zinaonesha kuwa nguvu na jitihada zaidi zinahitajika katika kuzuia maambukizi
mapya ya VVU kwa kuweka utaratibu thabiti na endelevu wa kutoa elimu na hamasa
ya kutumia huduma zilizopo za kupambana na UKIMWI nchini. “Kwa hiyo, programu
za kinga zinapaswa kuwa endelevu kwenye mikoa yote nchini, hususan mikoa yenye
kiwango cha juu cha maambukizi. Pia huduma za ARVs ziendelee kupewa kipaumbele
katika mipango yetu,” amesisitiza.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza
na washiriki wa hafla hiyo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto, Bi. Ummy Mwalimu alisema Tanzania kwa sasa ina watu karibu milioni
moja ambao wako kwenye matibabu ya kufubaza VVU.
“Kutokana na mpango wa PEPFAR, Tanzania
imekwishapokea sh. trilioni 10 tangu mfuko huu uanzishwe mwaka 2003 na matumizi
ya dawa za kufubaza VVU yamesaidia kupunguza idadi ya vifo vitokanavyo na
UKIMWI kwa asilimia 70, yaani kutoka vifo 110,000 mwaka 2003 hadi kufikia 33,000
mwaka 2016,” alisema.
Alisema kutokana na matumizi ya dawa
hizo, maambukizi mapya kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto nayo pia yamepungua
kutoka asilimia 12 na kufikia asilimia 4.9 hivi sasa.
Kwa upande
wake, Kaimu
Balozi wa Marekani, Bi Inmi Patterson alisema kati ya sasa na Septemba 2019,
PEPFAR inatarajia kutumia zaidi ya sh. trilioni moja (dola za Marekani milioni
512) katika kuboresha huduma za kuzuia maambukizi ya VVU, upimaji na matibabu
hapa nchini.
Alisema wanapoendelea na utekelezaji wa
kazi za mfuko huo na maadhimisho ya miaka 15 ya PEPFAR, kampeni yao itaendelea
kwa mwaka wote wa 2018 na imelenga kupunguza unyanyapaa na tabia ya kuwatenga
watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI.
“Kampeni ya PEPFAR15 inalenga kupunguza
unyanyapaa, kuongeza upatikanaji na matumizi ya huduma zitolewazo za kukabiliana
na VVU. Kila mtu atakayepimwa na kugundulika kuwa ana maambukizi ya VVU, ataanzishiwa
matibabu mara moja. Tutafanya kazi na watu wanaoishi na VVU nchini kote ili kusimulia
habari nzuri (positive stories) za watu wanaoishi na VVU ambao waliwahi kuwa
dhaifu ama wagonjwa lakini sasa wana nguvu na afya; habari za akinamama
wanaoishi na VVU na wanapata matibabu ili kuwalinda watoto wao,” alisema.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO,
MEI 30, 2018.
No comments:
Post a Comment